Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imefanikiwa kuwasajili washambuliaji nyota wawili kutoka Ghana, Samuel Afful na Yahaya Mohammed.
Zoezi la kuingiana
mikataba limehudhuria na baadhi ya viongozi wakuu wa timu wakiwemo Ofisa
Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Meneja Mkuu, Abdul Mohamed, Kocha Mkuu
Zeben Hernandez pamoja na wakala anayewasimamia wachezaji hao, Kingsley
Atakorah, ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Adom Wonders Academy ya
nchini Ghana.
Wakati Afful, 20, akisaini
mkataba wa miaka mitatu, Mohammed aliyetua nchini leo mchana akitokea
Ghana naye amesaini kandarasi ya miaka miwili tayari kabisa kuanza
kuitumikia timu hiyo yenye maskani yake Azam Complex, Chamazi, Dar es
Salaam.
Afful, 20, ambaye mpaka
sasa yumo katika vikosi vya timu za vijana za Ghana chini ya umri wa
miaka 20 na 23, anajiunga Azam FC akitokea timu ya Sekondi Hasaacan ya
Ghana, ambayo aliifungia mabao tisa timu hiyo msimu uliopita.
Moja ya rekodi yake ni
kuifungia bao muhimu timu ya Taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20
(U-20) mwaka jana dhidi ya Zambia kwenye ushindi wa mabao 2-1, lililoipa
nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini New Zealand, baada
ya kutinga nusu fainali ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana (U-20)
zilizofanyika Senegal mwaka jana.
Mohammed, 28, ambaye ni
mshambuliaji mzoefu anayetokea Aduana Stars, alikuwa ni mfungaji bora
namba mbili wa Ligi Kuu ya Ghana msimu uliopita akifunga mabao 15,
pungufu ya mabao mawili na kinara Latif Blessing (Liberty Proffessional)
aliyetupia 17.
Azam FC tunaamini ya kuwa
ujio wa nyota hao, utazidi kuipa nguvu timu yetu kuelekea kwenye
michuano inayotukabili mbeleni, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara (VPL), Kombe la Kagame (CECAFA Kagame Cup) tukiwa kama
mabingwa watetezi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na
Kombe la Shirkisho Afrika (CC) mwakani.
Azam FC tunapenda
kuwafahamisha mashabiki wetu kuwa tutaendelea kuyafanyia kazi
mapendekezo ya benchi la ufundi kwa kukifanyia marekebisho kikosi chetu
katika usajili huu wa dirisha dogo uliofunguliwa jana, lengo ni kukipa
nguvu zaidi kikosi chetu bili kifanye vizuri zaidi katika michuano ya
hapa nchini pamoja na ile ya Kimataifa.
Azam FC itaendelea
kuwathamini mashabiki wake na tunaamini ya kuwa uwepo wenu utaendelea
kutupa nguvu zaidi katika mapambano yetu makubwa ya kila siku na
yaliyoko mbele yetu, tunachowaahidi ni kuendelea kuwapa furaha zaidi kwa
kupata matokeo bora uwanjani na tunawaomba muendelee kuwa pamoja nasi.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
Bonyeza Hapa CLICK HERE
0 comments:
Post a Comment