Wednesday, 23 November 2016

#YALIYOJIRI>>>Chadema Kukusanya Bilioni 13.9 Kwa Mwaka Kupitia Kadi Mpya za Wanachama Zitakazoanza Kutolewa Mwakani.Fahamu zaidi hapa.

Chadema imetangaza kuwa Januari itaanza kutumia kadi mpya za uanachama za kielektroniki, zitakazoiwezesha kukusanya Sh13.9 bilioni kwa mwaka na kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali.

Mkakati huo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe wakati wa mkutano wa ndani uliofanyika mkoani Morogoro. Tofauti na Mbowe, viongozi wengine wa chama hicho walioko mikaoni ni Edward Lowassa aliyeko Dodoma na Frederick Sumaye ambaye yupo Singida.

Mbowe alisema mfumo huo utasaidia pia kudhibiti baadhi ya viongozi wasio waaminifu, wanaotumia mwanya wa kuuza kadi na kushindwa kuwasilisha fedha kwenye hazina ya chama.

Alisema kwa mfumo huo mpya, kama Chadema itakuwa na wastani wa wanachama 100,000 katika wilaya moja na kila mmoja kulipa ada ya Sh1,000 kwa mwaka, maana yake itaingiza Sh100 milioni.

Kwa hoja hiyo ya Mbowe, ikiwa chama hicho kitakuwa na wastani wa wanachama 100,000 katika kila wilaya za Tanzania Bara ambazo ni 139, Chadema itakuwa na uwezo wa kukusanya Sh13.9  bilioni kila mwaka.

Vyama vya siasa vinapata ruzuku kwa mujibu wa sheria na ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilibainisha kuwa jumla ya Sh67.7 bilioni zililipwa na Serikali kwa vyama vya siasa katika mwaka kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka wa fedha 2009/2010 mpaka 2012/2013. Fedha ambazo kwa mujibu wa CAG zilikuwa hazijakaguliwa kisheria.

Ikilinganishwa na mkakati mpya wa Chadema, fedha hizo ni ndogo katika kuhudumia shughuli za chama nchi nzima.

Mbowe alisema Chadema imeamua kuhakiki wanachama wake ili ifikapo Januari iwe tayari imemaliza kazi hiyo na kuingia rasmi katika mfumo mpya, utakaokisaidia kuondokana na dhana ya utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini.

Alisema ili chama kipige hatua na kuondokana na utegemezi wa ruzuku serikalini, wamekusudia kuingia katika mfumo wa kupata mapato kutoka ndani ya wanachama kupitia ulipaji wa ada.

Mbowe alizungumza na wanachama hao kutoka ngazi za vitongoji, vijiji, kata na wilaya waliohudhuria mkutano mkuu maalumu wenye lengo la kuwakumbusha mambo mbalimbali ya kuimarisha chama hicho baada ya Serikali ya Rais Magufuli kuzuia mikutano ya hadhara.

“Katika kipindi cha miaka miwili ijayo, Chadema itakuwa tayari imefanya utambuzi wa wanachama wake kwa kuwatambua katika kila mtaa, kitongoji, kijiji, kata na jimbo kupitia mfumo mpya wa kadi za eleketroniki ifikapo Januari 2017,” alisema Mbowe.

Alisema katika baadhi ya maeneo ya mikoa hapa nchini, kadi za uanachama za Chadema ni lulu na zimekuwa zikiuzwa hadi Sh5,000 badala ya 500.

Alieleza kuwa mapato ya chama lazima yatokane na ada za wanachama na siyo ruzuku ya Serikali, kwa kuwa utegemezi wa ruzuku ni hatari kwa uhai wake.

“Hii ruzuku inayotolewa na Serikali inatolewa kwa sababu ya CCM na CCM bila ruzuku hakiwezi kujiendesha,” alidai.

Mbowe alisema kila jimbo linapata fedha za ruzuku kulingana na idadi ya kura ilizopata katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, akitolea mfano Jimbo la Mlimba kuwa Mbunge Suzan Kiwanga alishinda kwa kura 40,000 wakati urais Chadema ilipata kura 38,000 huku katika udiwani wakipata kata tisa kati 16.

“Kutokana na ruzuku, Mlimba itapata Sh163,688 kila mwezi. Unaweza kuona fedha za ruzuku kutoka ndani ya chama ni ndogo sana ambapo Mkoa wa Morogoro unapokea kiasi cha Sh2.2 milioni kila mwezi.

“Kufikia mwaka 2017 kupitia programu ya Chadema msingi, tumekusudia kukijikita zaidi kusaka wanachama kutoka ngazi ya mitaa, vitongoji na balozi na tutaanza uchaguzi ndani ya chama.

“Tumebaini kuwa baadhi ya maeneo Chadema tumeshindwa kupata wenyeviti wa Serikali ya vitongoji na vijiji, kukosa madiwani na wabunge kutokana na kukosa misingi imara wa wanachama,” alisema Mbowe.


Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi


Bonyeza Hapa CLICK HERE

 

0 comments:

Post a Comment