Wakati
askari polisi saba watatoa ushahidi mahakamani katika kesi ya uchochezi
inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, Mahakama
imetoa onyo kwa askari Polisi na Magereza wanaowasumbua waandishi wa
habari na wananchi.
Onyo
hilo lilitolewa na Hakimu Mkazi Mfa- widhi wa Mahakama ya Mkoa wa
Arusha, Augustino Rwezile baada ya askari Magereza kuwafukuza kwa mbio
huku wakiwa na silaha waandishi wa habari waliotaka kuchukua kumbukumbu
za Lema kufikishwa mahakamani.
Pia, aliwaonya Polisi ambao wamekuwa wakilalamikiwa kwa kuwazuia wananchi wanapokwenda kusikiliza kesi ya mbunge wao.
Waandishi
wa habari jana waliwahi asubuhi kusikiliza kesi ya Lema na kutaka
kumpiga picha wakati akifikishwa mahakamani, lakini walipata wakati
mgumu baada ya kukimbizwa na askari Magereza wenye silaha ambao
hawakutaka mtu yeyote kupiga picha ya mtuhumiwa huyo.
Waandishi
hao, Lilian Joel (Uhuru) na Janet Mushi (Mtanzania) waliokolewa na
Hakimu Mkazi, Nestory Baro ambaye walimshika huku wakipiga kelele kuomba
msaada hatua ambayo ilizua tafrani mahakamani.
Hata
hivyo, baada ya tukio hilo, waandishi hao walipelekwa na hakimu Baro
kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Rwezile ambaye alishuhudia pia tukio hilo.
Hakimu
Rwezile aliwaita maofisa wa Polisi, waliokuwa mahakamani hapo na
kuwaonya kuacha tabia ya kuwakamata na kuwabughudhi wananchi na
wanahabari wanaofika mahakamani hapo kusikiliza kesi.
Hakimu
Rwezile, pia alilitoa agizo hilo la kuwaonya askari Magereza na Polisi
baada ya wakili wa Lema, John Mallya kuomba tamko la mahakama kutokana
na wananchi kuzuiwa kuingia mahakamani, kukamatwa na kunyanyaswa
waandishi wa habari.
Hakimu
Rwezile alitoa agizo tena kwa askari Magereza na Polisi wanaofika
mahakamani kuacha kuwasumbua wananchi na kueleza pamoja na wanahabari
wana uhuru wa kufika mahakamani na kusikiliza kesi.
“Hakuna
usiri mahakamani hatutarajii tena kuona misuguano hapa, tayari
nimezungumza na waandishi na askari Magereza kuhusiana na suala hili,
eneo hili lipo chini ya Mahakama hivyo watu wanapaswa kuingia na kutoka
salama,” alisema
Jana
saa mbili asubuhi, Lema alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa
Arusha kwa basi la Magereza, akiwa chini ya ulinzi mkali na
haikuruhusiwa kumpiga picha.
Mbele
ya Hakimu Rwezile, wakili wa Serikali, Fortunatus Mhalila alisoma
maelezo ya awali ya kesi hiyo na kudai upelelezi umekamilika na upande
wa Jamhuri una mashahidi saba.
Aliwataja
mashahidi hao kuwa ni Ofisa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Arusha (RCO),
SSP George Katabazi, Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Wilaya ya Arusha
(OSCID), ASP Damas Masawe, Mkaguzi wa Polisi, Adam Nyamiti, WP 6826
Ester Yohana na Ofisa wa Kitengo cha Upelelezi Makosa ya Mtandao Makao
Makuu ya Polisi, Ezekiel Kway.
Alidai
katika kesi hiyo, Lema anatuhumiwa kuhamamisisha watu kutenda kosa
ikiwa ni kinyume na kifungu 390 (35) cha Kanuni za Adhabu, iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Mhalila
alidai Lema kati ya Agosti Mosi hadi 26, alitengeneza na kusambaza
ujumbe mfupi wa sauti kupitia WhatsApp kuhamasisha watu kutenda kosa,
ikiwapo kuwataka kufanya maandamano kuanzia Septemba Mosi mwaka huu.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Rwezile alimtaka Lema kueleza kama maelezo
hayo ni sahihi au la.
Lema
alikanusha kutuma ujumbe wa kuhamamisha uvunjaji wa sheria. Wakili
Mallya alisema upande wa utetezi upo tayari kupangwa kwa siku ya kuanza
kuwasikiliza mashahidi. Kutokana na maelezo hao, Hakimu Rwezile
aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 2, ushahidi utakapoanza kutolewa.
Lema
na mkewe, pia wana kesi nyingine ya kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambayo nayo iliahirishwa hadi
Desemba 21 kutokana na mtuhumiwa wa pili, Neema Lema (33) kutokuwapo
mahakamani.
Wakili
Mallya alisema Neema ameitwa jijini Dar es Salaam katika kesi nyingine.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Rwezile aliahirisha kesi hiyo na Lema
kurejeshwa magereza hadi leo, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha itakapoanza
kusikiliza maombi ya dhamana.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
Bonyeza Hapa CLICK HERE
0 comments:
Post a Comment