Taasisi
ya The Desk & Chair Foundation (TD& CF), inatarajia kujenga
vyoo 100 katika Barabara Kuu ya Mwanza-Shinyanga-Dar es Salaam
unaokadiriwa kutumia Sh. milioni 500.
Mwenyekiti
wa TD & CF, Alhaji Sibtain Meghjee alisema hivi karibuni mjini
Mwanza kwamba mradi huo ni sehemu ya miradi mitatu mikubwa ambayo
taasisi yake inatekeleza nchini.
Alisema
baada ya kukamilisha mradi mkubwa wa jengo la kupumzikia wananchi
wanaokwenda kutibiwa na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure wanatarajia kujenga
vyoo 100 kwenye barabara ya kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam kwa basi.
Meghjee
alieleza kuwa maandalizi ya awali ya mradi huo yameshaanza na kwamba
watashirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu
(SUMATRA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ili kupata taarifa
sahihi kabla ya mradi kuanza.
“Penye
nia pana njia, baada ya kukamilisha ndoto yetu, leo ya mradi huu mkubwa
wa ujenzi wa jengo la kupumzikia hapa Sekou Toure, tunatarajiwa
kutekeleza miradi mitatu mikubwa ukiwemo wa vyoo kwa ajili ya abiria
wanaosafiri kati ya Mwanza na Dar es Salaam:
“Tunataka
msamiati wa kuchimba dawa wakati wa safari ubaki kuwa historia kwa hiyo
tunatarajia kufanya jaribio moja la kujenga matundu 100 ya vyoo katika
njia na barabara kuu ya Mwanza hadi Dar es salaam ambavyo vitagharimu
shilingi milioni 500.Tutashirikiana na mamlaka husika, ofisi yako na
idara ya afya,”alisema Meghjee.
Meghjee
alieleza kuwa taasisi hiyo pia ina mpango wa kutekeleza mradi wa
kutengeneza viungo bandia kwa kushirikiana na kitengo cha Jairpur
Foot/Knee and Limb Project cha India ambao unahitaji Dola 200,000 za
Marekani (sh. milioni 44), zitakazowezesha kuanzisha huduma ya viungo
hivyo bandia vya miguu, mikono, fimbo na baiskeli.
Alisema
wanaendelea kuwasiliana na wafadhili watakaoshirikiana nao kwenye mradi
huo na kuwahakikishia walengwa kuwa viungo hivyo vitapatikana kwa
gharama nafuu mara utakapokamilika mradi huo.
Meghjee
aliongeza kuwa wakati wakiendesha ujenzi wa jengo la mapumziko katika
Hospitali ya Sekou Toure,walipata wazo la kujenga mabanda yatakayotumiwa
na madereva wa pikipiki (boda boda) kuegesha vyombo vyao kivulini na
kupata huduma ya vyoo na mabafu.
Mwenyekiti
huyo wa TD & CF aliongeza zaidi kuwa endapo Halmashauri ya Jiji
itaridhia na kuwapa eneo maalumu na mahususi la ujenzi wa huduma hiyo
watafanya jaribio hilo moja ili kuweza kuona matunda yake.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
Bonyeza Hapa CLICK HERE
0 comments:
Post a Comment