Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP),Christopher Bageni amewasilisha maombi Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kupinga adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
SP
Bageni alihukumiwa adhabu hiyo baada ya mahakama hiyo kujiridhisha
kwamba aliwaua kwa kukusudia wafanyabiashara wanne wa madini kutoka
Mahenge mkoani Morogoro na dereva teksi mkazi wa Manzese, Dar es
Salaam, katika Msitu wa Pande.
Bageni
kupitia Wakili wake, Gaudioz Ishengoma, aliwasilisha maombi hayo
mwishoni mwa wiki yaliyoambatana na hati ya kiapo iliyoapwa na wakili
huyo.
Muwasilisha
maombi anaomba mahakama hiyo kuifanyia marejeo hukumu dhidi yake
iliyotolewa Septemba 13 na kusomwa Septemba 16 mwaka huu na Msajili wa
Mahakama hiyo, John Kahyoza.
Akitoa
sababu kuomba marejeo, anadai alinyimwa haki sawa ya kusikilizwa
wakati wa kutathmini ushahidi ulioko kwenye kumbukumbu za mahakama kwa
kuegemea kwenye ushahidi wa upande wa mashtaka.
Alidai
katika kuchanganua ushahidi ambao uamuzi wa mahakama uliegemea,
mahakama ilishughulika na ushahidi wa msingi (Exam in Chief) wa upande
wa mashtaka na iliangalia kwa juu juu tu ushahidi wa utetezi hususan wa
Bageni au haikuutazama kabisa.
“Kuna
kukinzana kwa haki kwa maana ya kwamba mtoa maombi alinyimwa haki sawa
ya kusikilizwa, kwa mahakama kuchagua na kuegemea upande wa mashtaka
pekee na kushindwa kuzingatia ushahidi wa upande wa utetezi, hasa wa
mtoa maombi.
“Uamuzi
wa mahakama umetolewa katika msingi wa makosa ya dhahiri kwenye
kumbukumbu za mahakama, hivyo kusababisha upotoshaji wa haki, kushindwa
kuzingatia mwongozo wa kanuni katika asili, thamani na matumizi ya
ushahidi wa kuungwa mkono,” ilisema sehemu ya maombi hayo.
Alidai
kuwa kwa kushindwa kuchanganua na kutathmini ushahidi kwa umakini
kwenye kumbukumbu, mahakama ilishindwa kuainisha ushahidi wa mjibu rufaa
wa nne (Bageni) kimazingira kama ilivyo ni dhahiri unakosa thamani ya
kuhitaji ushahidi wa kuunga mkono na hivyo si salama kuegemea katika
kumtia hatiani.
“Kwa
kushindwa kuona na kuzingatia ushahidi uliokusudiwa kuwa na ushahidi wa
kuunga mkono, siyo ushahidi huru na hauna mashiko kuthibitishwa (PW27)
na haupo (PW36).
“Kwa
kushindwa kufanya uchambuzi wa ushahidi kwenye kumbukumbu kwa umakini
wenye manufaa, vinginevyo mahakama ilipaswa kuona wajibu wa kuthibitisha
shtaka kwenye jinai haukufikiwa,”anasema Wakili Ishengoma.
Anadai
mahakama katika kuamua, kama ilivyofanya katika uhalisia wake, kuhusu
ushiriki wa mtoa maombi katika eneo la tukio la uhalifu, ilishindwa
kubaini katika ujumla wake ushahidi wa upande wa mashtaka ambao
haukuweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.
Ishengoma
alidai mahakama haikuuchukulia ushahidi kwenye kumbukumbu katika ujumla
wake hivyo kutengua uamuzi wa kuachiwa huru kwa mtoa maombi na kumtia
hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kusimamia ushahidi ambao haupo
na uvumi pamoja na ushahidi wa mashaka makubwa.
Alidai
kutokana na hukumu ya mahakama, haikuwa bayana ni kwa ushahidi wa nani
ulithibisha mtoa maombi Bageni alimwezesha au kumsaidia nani katika
mauaji ya marehemu hao.
Katika
hati ya kiapo iliyoapwa na Wakili Ishengoma, Bageni anadai yeye na
wengine wanane ambao hawako katika maombi hayo walishtakiwa Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam kwa makosa ya mauaji ya watu wanne katika Kesi
ya jinai namba 26 ya mwaka 2006.
Bageni
alikuwa mshtakiwa wa pili na katika hukumu iliyotolewa na Jaji Salum
Massati, amnayo wote waliachiwa huru, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP) hakuridhishwa na uamuzi huo hivyo alikata rufaa namba 358 ya mwaka
2013.
Kabla
ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, DPP aliwaondolea rufaa wajibu rufaa
watano na kubaki wajibu rufani wanne ambao waliachiwa huru pia Septemba
16, mwaka huu.
Walioachiwa
huru ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO)
Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na maofisa wengine wawili
baada ya mahakama kuona hakuna ushahidi wa wazi ama mazingira kuwatia
hatiani.
Katika
kesi ya msingi, Bageni alidaiwa kuwaua kwa kukusudia wafanyabiashara
Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi,
Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, aliyekuwa dereva wa teksi wa Manzese ,
Januari 14, mwaka 2006, katika Msitu wa Pande, Mbezi Luis, Dar es
Salaam.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
Bonyeza Hapa CLICK HERE
0 comments:
Post a Comment