Mwanasiasa
mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amesema bila ya kuwa na tume
huru ya uchaguzi na Katiba Mpya, vyama vya upinzani visahau kushinda
urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Kauli
ya Kingunge imekuja siku moja baada Rais John Magufuli kumteua Jaji
Themistocles Kaijage kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) baada ya Jaji Damian Lubuva kufikia muda wake wa kustaafu.
Kwa
muda mrefu, NEC imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kwa
kutokuwa huru kwa sababu ya uongozi wake wote huteuliwa na Rais ambaye
pia ni mwenyekiti wa CCM, huku sheria zikikataza matokeo ya nafasi ya
urais kupingwa mahakamani.
Mbali
na mwenyekiti kuteuliwa na Rais, wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ni
wakurugenzi wa wilaya ambao pia huteuliwa na Rais kwa kuwa NEC haina
wafanyakazi wake kote nchini.
Akizungumza
katika mkutano wa kuwafariji vijana waliokamatwa na Jeshi la Polisi na
kushtakiwa kwa makosa yaliyohusu Uchaguzi Mkuu uliopita, uliofanyika
jijini Dar es Salaam jana, Kingunge aliwatia moyo vijana hao, akisema
hakuna ushindi unaopatikana bila kupambana.
Kingunge,
aliyetumia muda mrefu kueleza historia ya maisha yake katika siasa na
jinsi alivyopambana katika harakati za kudai uhuru, alisema hali ya sasa
ni mbaya kuliko wakati wa wakoloni wa Kiingereza ambao walikujwa
wakali, kwa sababu CCM haifuati Katiba wala sheria.
“Yako
mambo ambayo itabidi tujitahidi yaamuliwe sasa kabla ya 2020. Mambo
hayo makubwa kwanza ni tume huru (ya uchaguzi). Suala hilo lazima
lizungumzwe sasa, hatuwezi kwenda 2020 na tume ya sasa na Katiba ya
mwaka 1977. Tukienda hivyo sahau habari ya upinzani kushinda uchaguzi,” alisema.
Kingunge
ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo ya waziri
anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na
mkuu wa mkoa alisema, “(Pia) Sheria inayohusu matokeo ya uchaguzi wa
Rais kuhojiwa. Hivi sasa sheria inasema matokeo ya uchaguzi wa Rais
hayahojiwi mahakamani. Lazima hilo suala lipate jibu sasa. Kwa hiyo
Katiba na sheria iseme, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kuhojiwa
mahakamani. Tusipokuwa na hilo, tutakuwa na matatizo makubwa sana.”
Alisema
pamoja na kwamba Chadema inapendwa na wananchi wengi na Edward Lowasa
aliyegombea urais kwa tiketi chama hicho, anapendwa, bado ni vigumu
kushinda kwa sababu mfumo uliopo sasa.
“Tufanye
yoyote, lakini tuhakikishe, ama tunapata Katiba Mpya au vipengele hivi
vya sheria vinafanyiwa marekebisho. Kwa maoni yangu, kundi hili lililo
madarakani bila shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi, halitataka
mabadiliko,” alisema.
Alisema
enzi zao walifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitolea kwa nguvu na
wengine, na yeye akiwamo, waliacha kazi za mishahara mikubwa na kujiunga
na Tanu kupigania uhuru.
“Tulifanikiwa
kupata uhuru kwa sababu walijitoa mhanga. Wengi tu waliacha kazi, mtu
anamaliza chuo kikuu anasema sitaki kazi anaingia Tanu kusaidia. Kwa
hiyo tukawa na jeshi kubwa la vijana waliohakikisha nchi inapata uhuru,”
alisema.
“Ninyi
mnapambana katika mazingira magumu na wazee wenzenu walipambana katika
mazingira hayo. Haikuwa rahisi. Wapo wengi walitusaliti, wengine
hawakufanya lolote. Baba yangu tuligombana, nilipoacha kazi kwenda
kuitumikia Tanu. Miezi sita hatukuzungumza.”
Akizungumza
mkutano huo, Lowassa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,
aliwatia moyo vijana walioshtakiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015, akisema bado jeshi kubwa la vijana linahitajika.
“Yaliyopita
si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo. Si haki kusema unakwenda mahali
pengine, mwenzako amepasafisha, safisha pa kwako. Nimefurahia moyo huo.
Kama alivyosema Ngombale, tunataka jeshi kubwa zaidi, watu wengi zaidi,”
alisema Lowassa.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment