Leo December 30, 2016 Mbunge Zitto Kabwe kutoka Kigoma Mjini
(ACT-Wazalendo) kupitia akaunti yake facebook ametoa taarifa kuhusu
madeni anayodaiwa, kiwango cha mshahara wake wa mwaka, kiasi cha pesa
kilichopo benki, posho pamoja na mali zote anazomiliki.
Hiki kimeandikwa na Zitto Kabwe leo.
Ndugu Watanzania, Kama mnavyofahamu kuwa ibara ya 132(4) na (5) na
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria namba 13 ya mwaka 1995
inataka viongozi wote wa umma kujaza fomu za Tamko la Rasilimali na
Madeni. Tamko hilo huwasilishwa Sekretariat ya Maadili ya Viongozi kabla
ya mwisho wa kila mwaka. Kama nifanyavyo siku zote, nawajulisha rasmi
kwamba nimetimiza matakwa hayo ya katiba na sheria kuhusu Maadili ya
Viongozi.
Inafahamika kuwa Chama Cha ACT Wazalendo, kwa mujibu wa Katiba yake
na Azimio la Tabora, kimeelekeza kuwa Viongozi wake wote waweke wazi
kwa Umma Tamko la Mali, Madeni na Maslahi. Kwa kufuata masharti ya
Katiba ya Chama Cha ACT Wazalendo natangaza rasmi fomu zangu
nilizowasilisha Leo Sekretariat ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Ni matumaini yangu kwamba itafikia wakati Daftari la Rasilimali na
Madeni la Viongozi wa Umma litakuwa linawekwa wazi kwa Umma ili wananchi
waweze kujua Mali, Madeni na Maslahi ya Viongozi wao na pale ambapo
kiongozi ametoa habari zisizo sahihi au kuficha mwananchi aweze kutoa
Taarifa kwenye Sekretariat na Baraza la Maadili liweze kufanya kazi yake
ipsavyo.
Mfumo wa kuweka wazi Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma ni
mfumo endelevu na muhimu kwenye vita vita dhidi ya ubadhirifu na
ufisadi. Mataifa kadhaa duniani hutumia mfumo huu ( public disclosure of
leaders’ assets and liabilities) kuwezesha mapambano dhidi ya rushwa na
ufisadi. Nchini Uingereza na Kanada kwa mfano, daftari la matamko ya
Rasilimali na Madeni ya Viongozi lipo wazi kwa kila mwananchi kuona na
huuzwa kwenye duka la vitabu la Bunge.
Namsihi Sana Rais John Pombe Magufuli kusaidia kufanya mabadiliko
makubwa ya Sheria ya maadili ya Viongozi ili kurejesha na kuboresha
Miiko ya Viongozi katika kuimarisha vita dhidi ya ufisadi nchini. Rais
aliahidi kuweka wazi Mshahara wake alipokuwa anazungumza katika kipindi
cha 360 cha Clouds TV.
Ninamkumbusha afanye hivyo na pia aweke wazi
Mali, Madeni na Maslahi yake ya Kibiashara ili awe mfano kwa Viongozi
wengine Nchini.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kigoma Mjini
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment