Stara Sudi, mke wa Saidi Mrisho ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala, jinsi alivyoshtuka baada ya kupokea simu aliyopiga mumewe kuwa amevamiwa na kuchomwa visu machoni, mgongoni na tumboni.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga
kutoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa Salum Njwete (34) maarufu ‘Scropion’,
Stara alimueleza Hakimu Mkazi, Flora Haule kuwa Septemba 6, saa tano
usiku akiwa amelala alipokea simu yenye sauti ya mumewe ikieleza kuwa
amevamiwa.
“Aliniambia mama Nancy nimechomwa visu hata kuona sioni hapa
nilipo nipo Buguruni,” alidai Stara ambaye ni shahidi wa pili wa upande
wa mashtaka.
Alidai tangu wafunge ndoa na mumewe Oktoba 2015 , Said
alikuwa akifanya kazi ya kinyozi katika saluni ya Rodgers iliyopo Tabata
Sanene.
“Baada ya kuongea na mume wangu, simu ilikatika lakini wakati
natafuta nguo nivae simu ileile ilipiga na nilipopokea sauti ya mtu
mwingine iliongea ambaye ndiye mwenye simu na aliniambia kuwa mume wangu
ana hali mbaya hivyo nifanye haraka niende Hospitali ya Amana,” alidai
Stara.
Baada ya kupata taarifa hizo, alidai alimweleza mtoto wao
mkubwa, Abdul Said (12) kuwa anaelekea Amana. Lakini kabla ya kwenda
huko alichukua pikipiki na kwenda Mabibo Hosteli anakoishi mama mkwe
wake kumweleza taarifa hiyo na kwamba waliambatana hadi Amana.
Alidai
wakiwa njiani, walimjulisha mdogo wa Saidi, Yahaya Kisukari (23) kuwa
kaka yako amepata matatizo ya kuvamiwa na mtu akachomwa visu na yupo
Hospitali ya Amana.
“Tulipofika Amana, tuliruhusiwa kuingia wodini na
kumuona mume wangu akiwa amefungwa bandeji machoni na sehemu nyingine za
mwili, huku damu ikivuja sehemu mbalimbali za mwili. Hata nguo aliyovaa
ilikuwa imejaa damu,” aliiambia Mahakama na kuongeza: “Baada ya kumvua
nguo zilizo- kuwa zimetapakaa damu, tulipewa rufaa kwenda Muhimbili kwa
ajili ya matibabu na wakati huo ilikuwa imeshafika saa sita usiku.”
Stara alidai baada ya kumuona mumewe aliyechomwa visu na mtu aliyemtaja
kwa jina la Scorpion, alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Buguruni.
“Baada ya kutoa maelezo Polisi Buguruni na askari kwenda kuchukua
maelezo ya mume wangu Muhimbili, tulikwenda kumkamata mshtakiwa Salum
Njwete,” alidai.
Alidai: “Septemba 8, tulirudi tena Muhimbili na kupewa
taarifa na daktari wa macho aliyemfanyia upasuaji Said kuwa macho yake
hayataona tena.” Stara alidai tangu waoane na mumewe, hajawahi kupata
malalamiko yoyote kuwa mwenza wake huyo ni mwizi.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment