JESHI
la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu 12, wakiwemo viongozi wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Arusha.
Viongozi
hao walikamatwa kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo
wakituhumiwa kuhusika kuchoma moto mashine za kuvuta maji kutoka kwenye
chanzo cha Kangdet wilayani Karatu kwa madai kwamba wanatekeleza agizo
la Serikali, hatua ambayo imeelezwa kuwa haikufuata utaratibu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha, Charles Mkumbo, aliwataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Moshi Darabe ambaye pia ni
Diwani wa Kata ya Barai, anayedaiwa kuhamasisha wananchi kuchoma moto
mashine hizo zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 16.
Wengine
waliokamatwa ni Diwani wa Kata ya Mang’ola, Lazaro Emanuel, viongozi wa
vijiji vya kata hizo pamoja na baadhi ya wananchi.
Kamanda
Mkumbo alisema kuwa msako wa kuwakamata watuhumiwa wengine waliohusika
na tukio hilo bado unaendelea na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa
mahakamani kwa hatua za kisheria.
Desemba
27, mwaka huu, kundi la wananchi wa vijiji vinne vya kata hizo
waliandamana, wakang’oa na kuchoma moto mashine za kuvuta maji katika
chanzo cha maji cha Kangdet, kinachotegemewa na vijiji vingine vya
Kata ya Barai.
Kutokana
na tukio hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa na
mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo, walitembelea
eneo la tukio na baada ya viongozi kueleza kilichotokea, aliagiza
kukamatwa kwa watu wote waliohusika na uharibifu huo.
“Sheria
lazima ichukue mkondo wake kwani agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
lilikuwa wazi na halikusema wananchi wachukue sheria mkononi, jambo hili
ni kinyume cha sheria,” alisema Gambo katika mkutano huo.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Jubilate Mnyenye (Chadema), amesema
kuwa yeye, mbunge wa jimbo hilo, Willy Qambalo na Mwenyekiti wa Kijiji
cha Mang’ola, Jacob Pius, wametakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi
jijini Arusha leo asubuhi kwa mahojiano kuhusu tukio hilo.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment