MKAZI wa kitongoji cha Upangwani, Kijiji cha Dodoma Isanga, Kata
ya Masanze, wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Augustino Mtitu,
aliyechomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni, amemshukuru Mungu,
madaktari, uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa na wananchi wa
kijiji hicho kwa kuwezesha kunusuru maisha yake.
Mkuki huo ulimjeruhi na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro kufanyiwa upasuaji na kufanikiwa kuondolewa mkuki huo na
kuokoa maisha yake.
Mtitu (42) ambaye ni mkulima alisema hayo alipokuwa akizungumza
na mwandishi wa habari hizi akiwa wodi namba moja, inayolaza wagonjwa wa
majeraha ya ajali katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro.
Mkulima huyo na wengine wanane walijeruhiwa katika vurugu
zilizohusisha jamii ya wafugaji wa kimasai na wakulima wa kijiji hicho
kilichopo katika wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Tukio hilo lililotokea saa 5:00 asubuhi Desemba 25 mwaka huu.
Alisema licha ya sasa kuendelea vizuri, alipata maumivu makali
kuanzia muda wa kuchomwa mkuki huo na kulazimika kuushikilia mkononi
mkuki kuanzia muda huo hadi saa 10:00 jioni ya siku hiyo alipofikishwa
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na madaktari kumfanyia
upasuaji na kuutoa.
“Namshukuru Mungu, pia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe
Stephen, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Frank Jacob waliofika kuniona na
kunifariji na leo (jana) amenitembelea Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule na
baadhi ya ndugu zangu wa kijijini Dodoma Isanga,” alisema.
Hata hivyo, hakuweza kuzungumza mwa muda mrefu kutokana na
sehemu ya jeraha bado ikiletea maumivu, ingawa alisema si kama
yaliyokuwa siku ya kwanza baada ya upasuaji.
Katika wodi hiyo, wananchi waliokuwa wakienda kuwaanglia ndugu
zao waliolazwa walikuwa wakimiminika eneo la kitanda chake wakimjulia
hali na kumpa pole kwa mkasa huo wa aina yake.
Naye Stanley Andrea, ndugu wa Mtitu, ambaye yupo katika
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro akimuunguza nduguye, alisema hali
yake inaleta matumaini ya kupona na kwamba kwa sasa anaweza kula
vyakula laini.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment