MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hawezi kufika
mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kwa kuwa
hajapokea barua ya kuitwa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Makonda alisema hatoweza
kwenda mbele ya kamati hiyo bila barua rasmi iliyomtaka kufanya hivyo.
Bunge lililokuwa likiendelea na vikao vyake Dodoma kabla ya
kuahirishwa juzi, lilipitisha uamuzi wa kuwataka Makonda na Mkuu wa
Wilaya ya Arumeru, Alaxander Mnyeti, kufika mbele ya kamati hiyo na
kuhojiwa kutokana na kauli walizozitoa, zinazodaiwa kuudharau mhimili
huo wa dola.
Lakini Makonda alisema jana “hilo suala la mimi kuitwa kwenye kamati nalisikia na kulisoma kwenye magazeti.”
“Sina uhakika ni lini wamefikia uamuzi huu wa kuniita na hata kama wamefikia uamuzi huo, sijaletewa barua rasmi.”
Baada ya Bunge kupitisha uamuzi huo wa kuitaka Ofisi ya Bunge
iwaandikie barua viongozi hao, juzi baadhi ya wabunge walihoji kauli ya
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, kwamba azimio la chombo hicho
cha kutunga sheria kumtaka Makonda kufika mbele ya kamati kujieleza
kuhusu tuhuma za kuudharau mhimili huo, halikufuata utaratibu.
Hatua hiyo iliamsha hasira kwa baadhi ya Wabunge na kuomba mwongozo
kuhoji kwa nini Katibu wa Bunge ametoa kauli ambayo inakinzana na
makubaliano ya Bunge.
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na mwezake wa Iringa Mjini
Mchungaji Peter Msigwa (wote Chadema) walihoji kuhusu kauli ya Dk.
Kashililah.
Waitara alisema, “Asubuhi ya leo ( juzi) nimetumiwa ‘clip’ ya sauti
ya Katibu wa Bunge akikosoa uamuzi wetu hapa na pia gazeti la Habari
Leo, Ukurasa wa 25, kuna habari imeandikwa.
Katika taarifa hii, Katibu wa Bunge anasema maazimio ya Bunge
yalikosewa na hayakufuata utaratibu,” alisema na kuongeza kuwa: “ Kwa
maana nyingine, hatatekeleza kile tulichokubaliana.”
Mchungaji Msigwa wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, alieleza kuwa hajafurahishwa
na kauli ya Katibu wa Bunge.
Alisema Katibu wa Bunge amekosea kwenda katika vyombo vya habari na
kudai chombo hicho cha kutunga sheria kimekosea kwa kuwa anafanya kazi
ya Bunge na kwamba hajaajiri wabunge na anapaswa kufuata maagizo yao.
Hoja ya kutaka kina Makonda washughulikiwe iliwasilishwa na Mbunge
wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) katikati ya wiki na ilijadiliwa na
kuungwa mkono na wabunge wote, wakiwamo mawaziri kwa kusema ‘ndiyo’.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment