Saturday, 13 May 2017

Waziri Mwakyembe aipongeza Klabu ya Afrika Lyon.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameupongeza uongozi wa Klabu ya michezo ya Afrika Lyon kwa kutumia mchezo wa mpira wa miguu kuelimisha jamii kupambana na ujangili wa tembo.

Mtendaji Mkuu wa Klabu ya afrika Lyon Bw.Rajuu Kagenzi (kushoto) akiongea wakati wa kikao na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe.
 
Waziri Mwakyembe ametoa pongezi hizo leo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na uongozi wa klabu hiyo katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO.

Katika kikao hicho uongozi wa timu hiyo ulimueleza Waziri kuwa timu yao imeamua kushiriki vita dhidi ya vitendo vya mauaji ya tembo kwa kuandika ujumbe maalum katika jezi za timu hiyo kuelimisha jamii dhidi ya vitendo hivyo.

“Ni jambo zuri kuhakikisha jamii inapata burudani ya mpira wakati huo huo inaelimika kupitia ujumbe unatolewa na wachezaji katika jezi zao”Dkt Mwakyembe alisema.

Kwa hivyo, aliushukuru uongozi wa timu hiyo kwa juhudi zao hizo na kukieleza kitendo hicho kuwa ni “cha mfano na kujivunia”.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia)akionyeshwa michora ya ramani za viwanja vya michezo vinavyotarajiwa kujengwa kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya afrika Lyon Bw.Rajuu Kagenzi(kushoto) leo Jijini dar es Salaam.
 
Aliongeza kuwa Serikali inajivunia na kuthamini mchango wa wananchi wazalendo wanaojitolea kujenga taifa na kulinda rasilimali zake kama timu ilivyofanya timu hiyo.

Aidha Waziri Dkt. Mwakyembe aliongeza kuwa ni jambo jema linalofanywa na klabu hiyo katika kuhakikisha inakuza na kuendeleza vipaji kwa vijana mbalimbali nchini jambo ambalo linasaidia kuinua sekta ya michezo.

Pia aliwapongeza kwa kupata fursa ya kutembelea nchi ya China kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu michezo na kuwataka kuitumia fursa hiyo ipasavyo kwa kujifunza kwa bidii ili watakaporejea waweze kufundisha vijana wengine wa kitanzania.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe(kulia) akipokea jezi kwa niaba ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya afrika Lyon Bw.Rajuu Kagenzi(kushoto) 
 
Naye Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Afrika Lyon Bw. Rajuu Kangezi ameeleza kuwa mkakati wa klabu hiyo ni kuhakikisha kuwa inajenga viwanja vya michezo vya kisasa kwa matumizi ya jamii ili kuendeleza michezo nchini hivyo ameomba ushirikiano na serikali katika kufanikisha mikakati hiyo.

“Tuna mipango mingi ya kuhakikisha tunakuwa na viwanja vizuri vya michezo na hili haliwezi kufanikiwa bila kuishirikisha serikali na viongozi wake hivyo tunaomba ushirikiano wa serikali katika kuhakikisha tunafanikisha jambo hili”

Katika kikao hicho uongozi wa klabu hiyo ulimkabidhi Waziri Mwakyembe jezi namba tano “5” ya klabu hiyo kwa ajili ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment