MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imesema Waziri wa Habari, Dk. Fennela Mkangara hakufuata utaratibu wa kisheria katika kulifungia gazeti la MwanaHALISI Julai 30 miaka mitatu iliyopita. Anaandika Erasto Stanslaus … (endelea).
Jaji Salvatory Bongole amesema Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 aliyoitumia kufungia gazeti hilo lililokuwa linachapishwa kila Jumatano na kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL), inaelekeza kuwa pamoja na hatua nyingine kutaka maelezo ya utetezi kwa mchapishaji.
Katika uamuzi wa shauri lililofunguliwa mara baada ya MwanaHALISI 
kufungiwa, Jaji Bongole amesema gazeti hilo liko huru kuchapishwa 
kuanzia sasa.
Jaji huyo amesema pamoja na uamuzi huo, kampuni iliyolalamika imepewa
 mafao yote iliyoyaomba katika kufungua shauri hilo la mapitio ya uamuzi
 wa Waziri – prerogative orders.
Miongoni mwa maombi ya faida ni HHPL kulipwa gharama za kesi pamoja 
na fidia kutokana na hasara iliyopatikana kwa muda wote wa gazti hilo 
kuwa kifungoni.
Wakati Waziri alipofungia gazeti la MwanaHALISI, alieleza kwamba sababu ni kuandika habari na makala za uchochezi.
Habari hasa iliyoikera serikali hata kujilazimisha kuchukua hatua 
hiyo katili, ilikuwa ni iliyohusu uchunguzi wa tukio la kutekwa na 
kuteswa hadi karibu na kifo kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha 
Madaktari Tanzania (TMA), Dk. Steven Ulimboka.
Dk. Ulimboka alikumbwa na mkasa huo mnamo Juni 2012 alipotekwa usiku 
eneo la Tazara, karibu na viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, ambako 
aliitwa na mtu aliyemtaja kuwa ni ofisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ambaye 
alikuwa na mawasiliano ya karibu naye kwa saa kadhaa siku chache na 
usiku huo siku ya tukio.
Daktari huyo aliyekuwa mtumishi wa taasisi ya Marekani nchini, 
alifika eneo la Tazara akifuatana na daktari mwenzake aitwaye Deo, 
ambaye mara baada ya tukio hilo, wakati wa alfajiri, alimpigia simu 
Mhariri wa MwanaHALISI, Jabir Idrissa, kumjulisha kuhusu kutekwa kwa Dk.
 Ulimboka.
Kufuatia habari za kuachiwa huru kwa MwanaHALISI, Mhariri huyo 
amesema amefurahishwa na uamuzi wa mahakama ya Tanzania, kwa kuwa 
umethibitisha kosa la serikali la kujichukulia maamuzi mkononi chini ya 
kuvunja sheria ilizoahidi kuzilinda.
“NImefurahi sana kuthibitishiwa kwamba serikali ilikosea katika 
kufungia gazeti. Uamuzi wa jaji umesema waziri hakufuata hatua za 
kisheria alizopaswa kuchukua kabla ya kufungia gazeti, ikiwemo ya kuwapa
 wamiliki na mhariri nafasi ya kujitetea,” amsema Idrissa.
“Lakini pia uamuzi huu unatakiwa uwe funzo muhimu kwa utawala kwamba 
hauwezi kudumu na kudumu kwa msisitizo wa kuhifadhi na kufurahia sheria 
zilizopitwa na wakati ambazo miaka kadhaa nyuma zilishatangazwa kuwa ni 
sheria kandamizi,” alisema.
Mhariri amesema anawasiliana na mmiliki na mchapishaji wa 
MwanaHALISI, kampuni ya HHPL, kukamilisha taratibu za kuchapisha toleo 
la kwanza haraka iwezekanavyo. Gazeti hilo lilikuwa likichapishwa mara 
moja kwa wiki siku ya Jumatano.
Kwa muda wote ambao gazeti hilo linatumikia kifungo, viongozi 
waandamizi serikalini, akiwemo rais Jakaya Kikwete, wamekuwa wakitamba 
kuwa hawatavumilia gazeti linalochapisha habari za uchochezi.
Waziri huyo aliyefungia MwanaHALISI anagombea ubunge katika jimbo la 
Kibamba, akikabiliana na ushindani mkali wa John Mnyika (Chadema) ambaye
 ni mwakilishi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Mkurugenzi Mtendaji wa HHPL, Saed Kubenea yeye anagombea ubunge jimbo la Ubungo kupitia Chadema pia akiwakilisha UKAWA
Chanzo 
                                        MwanaHALISI













0 comments:
Post a Comment