UTANGULIZI
1.
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeshtushwa na kusononeshwa na hatua
ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Nape Nnauye KULIFUTA katika daftari la Msajili wa Magazeti, Gazeti la
Mawio.
2.
TEF inaichukulia hatua hii kama aina mpya ya ukandamizaji wa uhuru
vyombo vya habari nchini. Kwa serikali zilizopita, tulikuwa tukipambana
na vitendo vya kufungiwa kwa magazeti kwa muda maalum, wakati adhabu
kubwa iliyowahi kutolewa ilikuwa ni ile ya kufungiwa kwa muda
usiojulikana kwa Gazeti la Mwanahalisi, kabla gazeti hilo kurejeshwa kwa
umma na Mahakama.
3.
Uamuzi wa kulifuta Mawio (hata kama lilifanya makosa) umetufikirisha
sana. Tumetafakari kwa kina na kujiuliza kwamba pengine habari ambazo
ziliandikwa na gazeti hili, zilikuwa hatari kwa kiasi gani kwa nchi
kiasi cha kufikiwa uamuzi huo? Ni magazeti mangapi yatafuata kufutwa
baada ya Mawio ikiwa serikali itaendelea na ubabe wa aina hii?
4.
Ndiyo maana tunaiona hatua ya Serikali kulifuta Mawio kama aina mpya ya
ukandamizaji wa uhuru wa habari ambayo imeasisiwa na Serikali ya Awamu
ya Tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli. Tunajiuliza ikiwa kwa miezi
takriban mitatu tu tangu kuanza kazi kwa serikali mpya tayari imefuta
gazeti, itakuwaje katika safari ya miaka mitano (miezi 60) ambayo
atakuwa madarakani?
MSIMAMO WA TEF
TEF inapinga uamuzi wa serikali kulifuta Mawio kutokana na sababu zifuatazo:
1.
Zipo kasoro nyingi za kimfumo zinazosababisha uamuzi wa Serikali
kutokubalika. Hii haimaanishi kwamba vyombo vya habari havifanyi makosa,
la hasha; lakini hata pale vyombo hivyo vinapofanya makosa yoyote yale,
taratibu za kuyashughulikia ni kinyume kabisa cha misingi ya utawala
bora, haki na demokrasia.
2.
Mfumo wa sasa wa kushughulikia matatizo au kasoro za kitaaluma katika
vyombo vya habari ni kandamizi kwani unamfanya Waziri kuwa “Mhariri
Mkuu” na ana mamlaka ya kutoa adhabu kwa kuzingatia mtizamo wake, hata
kama mtizamo huo unakinzana na misingi ya taaluma.
3.
Tunauona uamuzi wa serikali kuwa na nia mbaya kwani hata katika taarifa
yake kwa umma, haikuweka wazi habari ambazo zimesababisha kufutwa kwa
Mawio. Badala yake taarifa ya serikali inatoa kauli ya jumla kwamba
wahariri wa gazeti hilo “wameonywa mara nyingi lakini wamekuwa
hawabadiliki”. Hakuna anayefahamu walionywa lini wala kuhusu nini?
4.
Utaratibu uliotumika kulifuta Mawio ni uleule wa matumizi ya Sheria
kandamizi ya Magazeti ya 1976 ambayo takriban kwa miaka 20 imekuwa
ikipigiwa kelele kutokana na kumpa mtu mmoja (Waziri) mamlaka ya kuamua
suala kubwa la kuwanyima watu wengi (kwa idadi yoyote) haki ya kupata
habari. Hii ni tofauti na taaluma nyingine ambazo Serikali inaziheshimu
kwa kupeleka masuala husika katika vyombo vya sheria au mabaraza ya
uamuzi.
5.
Kwa taaluma ya habari, Serikali bado imeendelea kujipa mamlaka ya
“kukamata, kushtaki, kusikiliza kesi, kuhukumu na kufunga” Maana kama
ilikuwa ni kesi iliyozaa hukumu ya kufutwa, basi uendeshaji wake
ulifanyika katika “mahakama ya siri”, na usiri huu matokeo yake ni
hukumu ya siri ambayo haikuwapa wahusuka kutoa utetezi wa kile
kilichokuwa kikilalamikiwa dhidi yao. Hakuna anayefahamu nani alikuwa
mlalamikaji katika kesi hiyo, utetezi wa washtakiwa ni upi na chombo
gani kilichopima uzito wa mashtaka dhidi ya utetezi na kutoa uamuzi!.
6.
Mfumo wa aina hii ni kichaka ambacho Serikali imekuwa ikikitumia
kufanya kile ambacho kimeandikwa katika taarifa ya Waziri kwamba
Wahariri wa Mawio walionywa mara kadhaa! Hivi walionywa na nani, wapi na
kwa sababu zipi? Kama kile kinacholalamikiwa kingekuwa kimefikishwa
katika chombo rasmi cha utoaji haki, kila kitu kingekuwa wazi kwa umma
kwamba mashtaka ni yapi na utetezi wa washtakiwa ni upi.
7.
Mwenendo wa aina hii wa kufuta magazeti iwe ni kwa muda siyo tu kwamba
inaathiri dhana nzima ya utawala bora, bali inaliweka Taifa katika
hatari ya kutumbukia katika uovu, hasa pale wenye dhamana watakapofanya
wapendavyo kwa kuwa tu vyombo vya habari vitakuwa vimezibwa midomo.
8.
Kwa kuwa hii inaonekana kuwa dhamira rasmi ya Serikali kutumia sheria
kandamizi kudhibiti demokrasia na uhuru wa habari, tunatoa mwito kwa
watawala wetu kutafakari upya suala hili na kuachana kabisa na dhamira
hiyo isiyokuwa na tija kwa nchi yetu.
IMETOLEWA NA
JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA (TEF)
DAR ES SALAAM
0 comments:
Post a Comment