Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Dk. Joyce Ndalichako
**
MWALIMU
wa shule ya msingi Ikombolinga, Peter Emma, ameeleza masikitiko yake ya
kudhalilishwa na Ofisa Elimu wa shule za msingi, Mohammed Msongo,
wilaya Chamwino kwa kumzaba makofi mbele za walimu wenzake.
Mwalimu
Emma anasema udhalilishaji aliofanyiwa na Ofisa elimu huyo kwa kupigwa
makofi mbele ya walimu wenzake unatokana na kuchelewa kufika katika
semina ya mafunzo ya KKK licha ya kuwa mwalimu huyo alikuwa anatoka
mbali na alikuwa hajalipwa fedha ya nauli.
Akielezea
tukio hilo Mwalimu Emma amesema kwa mujibu wa ratiba ya mafunzo ambayo
yalianza Januari 16, mwaka huu yalitakiwa kuanza saa mbili kamili lakini
yeye na wenzake zaidi ya 20 walifika saa 2:40 asubuhi.
Akiendelea
kuzungumza na waandishi wa habari mwalimu huyo amesema kwamba yeye na
walimu wenzake waliochelewa walimkuta ofisa elimu huyo na kuwazuia
kuingia darasani kutokana na kuchelewa kwao.
Amesema
Ofisa huyo aliendelea kuwakaripia na kuwataka waandike majina yao kwa
malengo kwamba wasihudhurie mafunzo hayo KKK ambayo yalikuwa yanawahusu
walimu wote wa darasa la kwanza na la pili.
“Wakati
najitetea kuwa tunatoka mbali na usafiri ni wa shida huku hatukuwa na
fedha, ofisa elimu alinizaba makofi na kunisukuma ukutani.
“Kitendo hicho kweli kimeniumiza na kunidhalilisha sana hata hapa najifunza lakini sina amani natamani kurudi nyumbani.
“Tuliandika
majina ya waliochelewa sijui tutalipwa au la maana tunatakiwa kulipwa
Sh. 55,000 kwa kila siku na nauli lakini mpaka sasa hatujalipwa mimi
sielewi kwa kweli nimefadhaika sana.
“Kama uongozi ni wa ubabe hivyo hakika kazi itakuwa ngumu sana kwani hali hii inavunja moyo,” amesema Mwalimu Emma.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Chamwino, Richard Masimba alipotafutwa
ofisini kwake amesema taarifa hizo hawana na watazifuatilia.
Masimba
amesema ofisi haina taarifa ya mwalimu kupigwa vibao na kusukumwa
ukutani na iwapo itathibitika hatua za kisheria na kinidhamu zitafanywa.
Mtuhumiwa
wa tukio hilo, Ofisa Msongo, alipoulizwa alikana na kukataa katakata
kuwa hajampiga kibao wala kumsukuma ukutani mwalimu huyo.
“Jumla ya walimu 348 wanapatiwa mafunzo kazini na mafunzo hayo ni kwa shule za msingi serikali 119.
“Ila
ni kweli wapo walimu waliochelewa badala ya kufika saa 2:00 kama
tulivyo kubaliana wao wamefika saa 2:40 hivyo walipoteza dakika 40 za
kipindi.
“Kutokana
na hali hiyo nililazimika kukaa na walimu wote waliochelewa yakiwa
makundi mawili na kuwapa maelekezo ili wasiendelee kuchelewa kwani kwa
kufanya hivyo hawawezi kufaidika na hayo masomo,” alijieleza Msongo.
Hata
hivyo Msongo amesema siku ya tukio ambalo inadaiwa alimpiga mwalimu
huyo alimshika shati kwa nyuma na kumvuta ikiwa ni hatua ya kutaka
asijichanganye na kundi lingine lisilomuhusu lakini siyo kumpiga.
Kwa
upande wake Katibu wa Chama cha Walimu (CWT), Wilaya ya Chamwino, James
Puya amesema analaani vikali kitendo cha ofisa elimu msingi kumzaba
mwalimu vibao.
“Kitendo hicho kinawafanya watumishi kukosa morali wa kufanya kazi kwa ufasaha na wakati mwingine kuhamishia hasira kwa watoto.
“Mimi
nimepata taarifa za mwalimu kupigwa na nasema kama kiongozi wa CWT
wilaya ya Chamwino kulikotokea hili tatizo naomba tume ya Haki za
binadamu, Mkurugenzi na Utumishi kuingilia kati suala hili.
“Unyanyasaji
huu usipokomeshwa haraka itakuwa mwendelezo wa viongozi wa ngazi ya juu
kuwanyanyasa watumishi wa ngazi ya chini jambo ambalo ni hatari,” amesema Puya.
0 comments:
Post a Comment