Tuesday, 12 January 2016

#YALIYOJIRI>>>Jecha wa ZEC Atoka Mafichoni.....Dk. Shein Asisitiza Uchaguzi Lazima Urudiwe Zanzibar.Fahamu zaidi hapa.

Hatimaye  Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, jana ameonekana hadharani katika maadhimisho ya sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi zilizofanyika kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja.

Jecha ambaye inaaminika alikuwa mafichoni tangu alipotangaza kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka jana, alionekana ameketi kwenye jukwaa kuu la viongozi, jirani na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Kuonekana kwa Jecha hadharani kumezua mijadala mitaani na hata katika mitandao ya kijamii, huku wengi wakihoji alikuwa wapi mara baada ya kufuta matokeo ya uchaguzi.

Watu mbalimbali wamekuwa wakihoji kuonekana kwa Jecha hadharani jana, siku ambayo Dk. Shein alitumia maadhimisho ya Mapinduzi kutangaza kwamba uchaguzi wa marudio Zanzibar iwe isiwe utafanyika.

Oktoba 28, mwaka jana majira ya saa sita mchana kwenye Ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar zilizopo Kilimani mjini Unguja, ilikuwa ndiyo siku ya mwisho kuonekana Jecha hadharani.

Siku hiyo huku akiwa chini ya ulinzi wa vijana wawili wanaoaminika kuwa ni makomandoo wa Jeshi la Ulinzi wa Tanzania (JWTZ) waliovaa kiraia, Jecha alitangaza kuufuta uchaguzi wa Zanzibar mbele ya vyombo vichache vya habari.

Alitumia dakika mbili tu kuvitangazia vyombo hivyo vya habari juu ya adhima yake ya kuufuta uchaguzi na kutoa sababu zilizomfanya kufanya hivyo ikiwamo kuharibiwa kwa uchaguzi kisiwani Pemba.

Hata hivyo, baada ya kumaliza kutoa taarifa yake kwa vyombo hivyo, Jecha hakutaka kuulizwa maswali.

Oktoba 27, mwaka jana ikiwa ni siku moja kabla ya kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi, Jecha pia hakuonekana kwenye kituo cha kutangaza matokeo kilichokuwa katika Hoteli ya Bwawani kwa kile kilichodaiwa alipata matatizo ya kiafya na hivyo kumwachia kazi hiyo Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa.

Siku hiyo majira ya saa kumi jioni, askari wa JWTZ walizingira kituo cha Bwawani na kuwaamuru watu waliokuwa ndani kutotoka nje na hata wale walioko nje ya kituo hicho kutosogea.

Watu waliokuwa ndani ya kituo hicho wengi wao walikuwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi pamoja na baadhi ya wawakilishi wa vyama vya siasa waliofika kusikiliza matokeo ya uchaguzi.

Dr. Shein asisitiza Uchaguzi lazima urudiwe
Kutokana na kile kinachoonekana kuendelea kupasuka kwa hali ya kisiasa visiwani Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza uchaguzi utarudiwa baada ya awali matokeo yake kufutwa na ZEC.

Akihutubia katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Uwanja wa Amaan jana, Dk. Shein alisema uchaguzi huo utarudiwa kwa mujibu wa katiba na sheria.

“Kila mmoja anajua kilichotokea katika uchaguzi Zanzibar baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi kutokana na kasoro zilizogundulika kutokea wakati wa uchaguzi huo,” alisema Dk. Shein na kuongeza:

“Suala la kurudiwa kwa uchaguzi liko palepale na utarudiwa kwa mujibu wa katiba na sheria, hivyo nawaomba wananchi muwe na uvumilivu na upendo wakati tukisubiri kutangazwa kwa tarehe ya kurudiwa uchaguzi.”

Licha ya kwamba kila upande umeshaweka msimamo wake, lakini Dk. Shein alisema mazungumzo ya kusaka suluhu yanaendelea baina ya pande hizo na kwamba taarifa ya mazungumzo hayo itatolewa punde yatakapokamilika.

“Tangu kutokea kwa mgogoro huu tulishauriana kukutana viongozi sita waliopo madarakani na waliostaafu ili kufanya mazungumzo ya kusaka suluhu na taarifa itatolewa pindi mazungumzo yatakapokamilika,” alisema Dk. Shein.

0 comments:

Post a Comment