Waziri
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako amefuta mfumo wa matokeo ya GPA kwa wanafunzi wa kidato cha
nne, sita na ualimu na kurudisha ule wa zamani wa divisheni.
Mbali na hilo, Ndalichako ameagiza kuondolewa kwa mtihani wa pili (paper two) kwa watahiniwa binafsi ambao ulianza mwaka 2014.
Katika
mkutano na waandishi wa habari jana, Profesa Ndalichako alisema
Serikali haitawavumilia watu ambao wanataka kuchezea elimu.
“Nilitembelea
Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Januari 7, nikaagiza wanipe sababu
za msingi za kutoka divisheni kuingia GPA, hadi leo wameleta maelezo
bila ya sababu za msingi na maelezo yao yamejikita katika blabla ambazo
hazijitoshelezi,” alisema Profesa Ndalichako ambaye katika mkutano
huo aliongozana na naibu wake, Stella Manyanya na Katibu Mkuu wa Necta,
Dk Charles Msonde.
Alisema
kuna mgongano mkubwa katika upangaji wa GPA kwani kidato cha nne ufaulu
unaanzia 3.6 -5, kidato cha sita katika daraja hilo wanaanzia 3.7 -5
wakati ufaulu kama huo kwa mafunzo ya ualimu unaanzia 4.4 -5 ambao ni
mkanganyiko mkubwa unaozalisha watu wasio na ubora wa kiwango husika.
“Baadhi ya watahiniwa waliopitia katika mfumo huo na kufaulu wanaonyesha kiwango kidogo cha maarifa kuliko kiwango cha ufaulu,” alisema.
Alisema
kuwapo gredi E kwenye alama za ufaulu wakati haihesabiki katika
upangaji wa GPA, kunawafanya watahiniwa waliopata E kujiona wako bora
kuliko wenye D mbili na F zote ambao wanahesabiwa wamefaulu.
Alisema
Necta imetoa maelezo mengi ambayo yameonekana hayana uhalisia wala wa
kukamilisha sababu badala yake wamejikita katika visingizio.
Alisema
Necta walimweleza kuingia katika mfumo huo ilikuwa ni maoni ya wadau
lakini alipowauliza ni wadau kiasi gani na mikutano hiyo ilifanyikia
wapi, hawakuwa na majibu na hakuna hata mkutano ambao uliwahi kufanyika.
“Jambo
jingine lazima mkumbuke kuwa, mfumo huu haujaenda hata kwa kamishna wa
elimu kupata kibali, ndiyo maana wadau waliniambia kuwa nisingetoa siku
saba badala yake ningeufuta mara moja,” alisema Ndalichako.
Alipinga
madai kwamba uliruhusiwa na Serikali, akisema ulianza kutumika tangu
2014 wakati maagizo ya Serikali Mtandao (EG) yalieleza kuwa kila kitu
kianze kutumika Juni 16, mwaka huu.
Alisema
alidanganywa kwa kuambiwa wizara iliagiza wakati amebaini kuwa wizara
ilipitisha kanuni za mitihani Oktoba 28, 2015 na kuingiza katika gazeti
la Serikali Novemba 6 mwaka jana ikiwa ni miaka miwili tangu mfumo wa
GPA uanze kutumika.
Kwa
upande wa watahiniwa binafsi, alisema kuanzia sasa hakutakuwa na
mitihani miwili ambayo mmoja ulikuwa ni kwa ajili ya upimaji endelevu,
hivyo watahiniwa watafanya mtihani mmoja tu.
Hata
hivyo, Dk Msonde alisema watahiniwa binafsi wa sasa watasahihishiwa
mitihani yao kwa mfumo wa mitihani miwili kwa kuwa walishafanya.
0 comments:
Post a Comment