Uongozi wa Simba umefikia uamuzi wa kuachana na Kerr baada ya
kutoridhishwa na mwenendo wa kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara na
baadaye Kombe la Mapinduzi baada ya kutupwa nje ya mashindano hivi
karibuni kwenye mashindano yanayoendelea visiwani Zanzibar.
Pamoja na kutokuwa na matokeo mazuri lakini inaonekana uongozi
haujaridhishwa na uchezaji wa kikosi cha timu hiyo na mambo yalikuwa
mabaya zaidi katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar.
“Kweli kamati ya utendaji imefanya kikao cha muda cha dharura na kukubaliana na hilo,” kilieleza chanzo kutoka Zanzibar.
“Taarifa tulizonazo ni kwamba kocha Kerr ameitwa Dar es Salaam ambako
ataondoka kesho (leo) Jumanne akiwa Dar es Salaam ataelezwa kuhusiana
na uamuzi huo wa uongozi kumtupia virago na nafasi yake atapewa Kocha
Majanja ambaye juzi aliingia mkataba kama kocha msaidizi”.
Chanzo kilipoulizwa kama uongozi hauwezi kubadili uamuzi hiyo kesho,
kilieleza: “Tunaamini hakuna nafasi hiyo, hata Kerr mwenyewe
ameishashitukia, atakuwa anajua kwamba mambo yatakuwa hivyo”.
Taarifa nyingine zimeeleza kwamba Kerr raia wa Uingereza ameponzwa na
ubishi na uongozi umekuwa ukimlaumu kutofanya kazi kwa kujituma.
Wakati fulani, Rais wa Simba, Evans Aveva aliwahi kujitokeza
mazoezini kimyakimya wakati Simba ikijifua kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu
Dar es Salaam (UDSM), hali iliyoonyesha wazi uongozi hauridhiki na
utendaji wa Mwingereza huyo aliyechukua nafasi ya Goran Kopunovic
aliyeondoka baada ya kutaka dau la Sh milioni 100 ili aongeze mkataba
mpya Simba.
Kerr anaondoka na kuiacha Simba katika nafasi ya tatu baada ya mechi
13 na imekusanya pointi 27 nyuma ya Yanga yenye 33 na Azam FC kileleni
ikiwa na 35.
Mwingereza huyo anaiacha Simba ikiwa imeshinda mechi 8, sare 3 na
kupoteza mbili, imefunga mabao 20 ikishika nafasi ya tatu kwa ufungaji
baada ya Yanga yenye 30 na Azam FC yenye 27 huku ikiwa imeruhusu mabao
9, ikiwa safu bora ya ulinzi katika nafasi ya nne baada ya Azam
iliyoruhusu mabao 8, Mtibwa Sugar mabao 7 na Yanga yenye safu ngumu
zaidi imefungwa mabao matano tu.
CHANZO: salehjembe.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment