Aliyekuwa
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA),
Philip Saliboko, ameachiwa huru katika shtaka la kutuhumiwa kuwa
alipokea rushwa ya Sh milioni 40.4 kutoka kwa Mkurugenzi wa zamani wa
Kampuni ya IPTL, James Rugemalira.
Saliboko aliachiwa jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kumuona hana hatia.
Hukumu
hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, aliyesema
mahakama imemuona mshtakiwa hana hatia kutokana na upande wa Jamhuri
kushindwa kuthibitisha shtaka dhidi yake pasi na kuacha shaka yoyote.
“Mahakama
inaona upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi bila ya shaka.
Mshtakiwa (Saliboko) hana hatia, anaachiliwa huru na mna haki ya kukata
rufani kwa upande ambao haujaridhika,” alisema Simba.
Alisema
mshtakiwa huyo aliposomewa shtaka kwa mara ya kwanza alikana na kwamba
wakati wa usikilizwaji upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa
Serikali, Dennis Lekayo, ulileta mashahidi watatu ambao ni mpelelezi
mkuu na maofisa wawili wa Benki ya Mkombozi iliyoko Ilala, Dar es
Salaam.
Pia alisema mshtakiwa anatetewa na Wakili Jamhuri Johnson, alijitetea mwenyewe baada ya mahakama kumuona ana kesi ya kujibu.
Hakimu
Simba alisema shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri alikuwa Mpelelezi
Mkuu, Emmanuel Koroso, aliyeeleza kuwa alikabidhiwa jalada afanye
upelelezi juu ya tuhuma hizo za Saliboko Oktoba 9, mwaka juzi na
Mkurugenzi wa Takukuru.
Akichambua
ushahidi wake, Hakimu Simba, alisema shahidi huyo alieleza alikusanya
hati mbalimbali na kuhoji watu na alijitosheleza fedha hizo ziliingizwa
katika akaunti ya Saliboko na mshtakiwa huyo hakuwa na maelezo mazuri
kuonyesha namna gani alipokea fedha hizo.
Alisema
mashahidi wawili kutoka Mkombozi, walithibitisha Saliboko alienda
kufungua akaunti kama mteja wao na fedha hizo ziliingizwa katika akaunti
ya mshtakiwa huyo na alizitoa mara tatu.
Kwa
upande wa utetezi wa mshtakiwa Saliboko, alikubali kufungua akaunti ya
Mkombozi na kuingiziwa fedha hizo na Rugemalira aliyekuwa na makubaliano
naye ya kumtafutia shamba katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam ili
aendeleze biashara zake.
Baada
ya kuchambua ushahidi huo, Hakimu Simba alisema utaratibu wa sheria ni
kwamba upande wa Jamhuri ndio wenye wajibu wa kuthibitisha mashtaka pasi
kuacha shaka yoyote na sio jukumu la mshtakiwa kuthibitisha kwamba
hajafanya kosa.
“Katika
kesi hii, hakuna ubishi kwa upande wa Jamhuri na ule wa utetezi kwamba
fedha ziliingizwa katika akaunti ya Saliboko, hivyo hakukuwa na ulazima
wa kuwaleta wale mashahidi wawili kutoka Benki ya Mkombozi.
“Shahidi
muhimu aliyebaki ni mpelelezi mkuu ambaye alipohojiwa na wakili wa
utetezi alidai hakuna siku hata moja alienda kumuuliza Rugemalira fedha
ziliingia katika akaunti ya Saliboko kwa kazi gani.
"Kwa
mujibu wa sheria za Takukuru, mtoa rushwa na mpokea rushwa wote ni
wakosaji, kama kweli ilikuwa rushwa kwanini Rugemalira hakuletwa
mahakamani kushtakiwa maana ni mtoaji,” alisema Hakimu Simba.
Kwa
mujibu wa hati ya mashtaka, Saliboko alikuwa anadaiwa Februari 5, mwaka
juzi katika Benki ya Mkombozi, iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam,
akiwa mkuu wa Rita alipokea Sh milioni 40.4 kupitia akaunti ya VIP
Engineering ya Rugemalira ambaye alikuwa Mkurugenzi wa IPTL.
Ilidaiwa alipokea fedha hizo kutokana na kazi yake kama bosi wa Rita wakati IPTL ilikuwa mfilisi na yeye alishughulikia hilo.
0 comments:
Post a Comment