Mahakama
ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imemuachia huru aliyekuwa Mbunge wa
Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila, baada ya upande wa mashtaka
kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani hapo kwa zaidi ya siku 60 kwa
mujibu wa kifungo cha 25 cha kanuni ya adhabu.
Uamuzi
huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Slivester
Kainda, katika kesi iliyokuwa ikimkabili Kafulila akidaiwa kutoa lugha
ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo.
Akitoa
uamuzi huo Kainda alisema: “Kesi hii ni ya muda mrefu sana na upande wa
mashtaka umeshindwa kuleta mashahidi na wakati mashahidi hao wanaishi
hapa Kigoma, hivyo kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuleta
mashahidi ninaifuta kesi hii”.
Hakimu
Kainda alifuta kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka ukioongozwa na
wakili wa serikali, Shabani Masanja, kudai mahakamani hapo kuwa haukua
na mashahidi na kuomba ipangwe tarehe nyingine ya kesi hiyo kutajwa.
“Mheshimiwa
kwa leo (jana)hatuna mashahidi, tunaomba mahakama yako tukufu ipange
tarehe nyingine ya kutajwa ili tulete mashahidi,” aliomba wakili huyo.
Awali
akisoma hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali, Shabani Masanja, alidai
kuwa, Agosti 1, mwaka 2013, majira ya jioni katika uwanja wa Rest
House, kata ya Nguruka, wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma, mshtakiwa akiwa
Mbunge akiwa kwenye mkutano wa hadhara alitoa lugha ya matusi dhidi ya
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Nyembo.
Alidai
mshtakiwa huyo akiwa kwenye mkutano huo wa hadhara, alitamka kuwa “Mtu
kama Hadija Nyembo unamuokota wapi na kumpa ukuu wa wilaya, unamchukua
shangingi la mjini uko unasema aliwahi kuwa mkuu wa wilaya, mkuu wa
wilaya akija hapa maana yake polisi wa wampigie saluti, kuna polisi
wenye akili hapa kuliko huyu mkuu wa wilaya, wanampigia saluti basi tu
manake hana hakili.”
Alidai lugha hiyo ilimdhalilisha mkuu huyo wa wilaya na kwamba kitendo hicho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Masanja
alisema upande wa mashtaka ulipanga kupeleka mahakamani hapo mashahidi
sita na kielelezo kimoja cha CD yenye maneno ya kashfa yaliyotolewa na
mshtakiwa.
0 comments:
Post a Comment