Wakati
vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vikitarajiwa kuanza leo kwa uteuzi
wa wajumbe, wabunge wa upinzani tayari wameanza kwa kumtikisa Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, baada ya kususia uchaguzi wa wenyeviti wa kamati hizo.
Dalili
za mgawanyiko kwenye kamati hizo zilianza kuonekana juzi, baada ya
wabunge hao wa Kambi ya Upinzani kufanya kikao na kuweka msimamo wa
kutaka kushirikishwa kwenye uteuzi wa wajumbe.
Kambi
ya Upinzani ilisema inataka kushirikishwa katika hatua hiyo ikidai
kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), imekuwa ikiwapangia watu wa kuongoza
kamati zinazosimamia mapato ya serikali ambazo kikanuni zipo chini yao.
Viongozi
hao wa kambi ya upinzani walidai kuwa kwa muda mrefu wamekuwa
wakipangiwa watu wa kuongoza Kamati ya Hesabu za Serikali za (PAC) na
ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ambazo kikanuni zinatakiwa
kuongozwa na upinzani.
Baada
ya Ofisi ya Bunge kutangaza majina ya wajumbe wa kamati, Kambi ya
Upinzani Bungeni ilikutana na waandishi wa habari, lakini wakaahirisha
kwa madai kuwa wamegundua kwamba orodha ya majina yaliyotoka, yana
matatizo mengi zaidi.
“Tumegundua
kwamba matatizo hayapo kwenye kamati ya PAC na LAAC tu, kwenye kamati
nyingi kuna matatizo kwa hiyo kwa sasa viongozi wa kambi wanakutana
kujadili na kuchambua taarifa iliyotolewa baadaye tutakutana na wabunge
wote kisha kesho tutatoa msimamo wetu,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Mnyika.
Baada ya kauli hiyo, Mnyika aliulizwa inakuwaje wao wanaendelea na vikao wakati wenzao wa CCM wakiwa kwenye uchaguzi:
“Siwezi
kujibu chochote, neno lolote nitakalosema, nitaingilia hicho
kinachojadiliwa na viongozi. Wewe subiri kwanza tumalize kikao, tutoke
na msimamo wa pamoja na kesho tutawaeleza msimamo wetu,” alisema Mnyika.
Awali,
kabla ya kutolewa kwa majina hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya, alisema kwa muda sasa wamekuwa
wakichaguliwa watu wa kuongoza kamati hizo na CCM.
“Ni
sawa na mtu anakupa kitu kwa mkono wa kushoto na kukunyang'anya kwa
mkono wa kulia. Ndiyo maana tukataka tushirikishwe kuanzia wajumbe
watakaokuwa kwenye kamati hizo,” alisema Sakaya ambaye ni Mbunge wa Kaliua mkoani Tabora.
==>Kauli ya Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Facebook
Kupitia ukurasa wake wa facebook, Zitto Kabwe ambaye bunge lililopita alikuwa mwenyekiti wa PAC ameandika;
"Kamati zote za Bunge zina hadhi sawa ndani ya Bunge. Kila mbunge ana haki ya kuwa kwenye kamati yeyote ile na hakuna mbunge bora zaidi ya mwingine.
"Kanuni zimeweka utaratibu wa uteuzi kwenye Kamati ikiwemo maombi ya mbunge, uzoefu na ujuzi wa eneo husika.
"Wanaolalamika
leo upangaji wa Kamati ndio usiku wa kuamkia jana walimshinikiza Spika
asiwapange mahasimu wao kisiasa kwenye Kamati wanazoona wao ni nyeti.
"Ni
unafiki uliopitiliza unapojenga hoja ya uzoefu, chaguo la Mbunge na
ujuzi wakati huo huo wenye vigezo vyote hivyo unawapiga vita kwa sababu
za kisiasa
"Ni
dhahiri kuwa mpangilio wa Kamati unajenga Bunge kibogoyo,
Nilitahadharisha toka Bunge la 11 lilipoanza kwamba, "kuna dalili za
Serikali kutaka kulidhibiti Bunge ( kumbukeni sarakasi za Tulia Ackson
ambaye sasa ni Naibu Spika) . "
"Kiongozi
unapokwenda kwa Spika kusema 'fulani asipangwe Kamati fulani kwa sababu
atapata sifa' halafu ukataka 'nyumbu' wako ndio wapangwe huko ujue
unaisadia Serikali kudogosha Bunge.
"Spika anapoamua Nyote, huyo usiyemtaka na nyumbu wako wasiende huko ujue amekudharau sana.
"Unapoona
Viongozi wa Serikali wanahangaika kupanga Kamati za Bunge watakavyo wao
ujue viongozi hao ni dhaifu, hawana nia njema na hawataki kuwajibishwa.
"Twendeni
kwenye hizi hizi Kamati tulizopangiwa kuwafanyia kazi Watanzania.
Twendeni tukaonyeshe kuwa Bunge litabaki Bunge tu na Wabunge tusikubali
Bunge Kibogoyo. Ni lazima Bunge lidhibiti Serikali hata Serikali hiyo
ikiwa inaongozwa na Malaika.
0 comments:
Post a Comment