Nyaraka
za ukaguzi wa kina uliofanywa na kampuni ya Philip& Company
imebaini kuwa Khalfan Kikwete ambaye ni mtoto wa rais mstaafu, Dk.
Jakaya Kikwete ni sehemu ya wamiliki wa kampuni ya Simon Group
iliyonunua UDA kwa bei ya kutupwa.
Taarifa
kutoka katika nyaraka hizo za ukaguzi zimebainisha kuwa hesabu za mwaka
2008 za kampuni ya Simon Group zilionesha kuwa Khalifan Kikwete ni
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo pamoja na Robert Simon Kisena.
Imeelezwa
kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliiuzia kampuni hiyo hisa za
UDA bila kufuata utaratibu na sheria huku hesabu zake zikionesha utata
mkubwa.
Ukaguzi
huo ulionesha kuwa Simon Group haikuwa na uzoefu katika biashara ya
usafirishaji wa abiria. Lakini pia hesabu zake za mwaka 2007
zilishangaza baada ya kuonesha kuwa ilipata faida ya shilingi bilioni 1
baada ya kufanya kazi kwa mwezi mmoja tu (Kuanzia Novemba 2007 hadi
Desemba 2007).
Hesabu
hizo zilichanganya zaidi baada ya kampuni hiyo kuonesha kuwa na hesabu
za mwaka mzima wa 2007 wakati imesajiliwa na kuanza biashara mwezi
Novemba 2007. Taarifa yake ya hesabu pia haikuonesha kuwepo kwa uchakavu
ili hali inamiliki vifaa kama magari na kompyuta.
Katika
hatua nyingine, Ukaguzi huo umebaini kuwepo kosa la jinai kwa kampuni
hiyo ya Simon Group kukwepa kulipa kodi. Kati ya faida ya shilingi
bilioni 1.7, walilipa kodi ya shilingi 225,000 tu, kinyume cha sheria ya
kodi inayoitaka kampuni kulipa asilimia 30 ya faida iliyopata, ambayo
kwa Simon Group ingekuwa shilingi milioni 510.
Hata
hivyo, Robert Simon Kisena aliyetajwa kuwa mmoja kati ya wakurugenzi wa
kampuni ya Simon Group alipoulizwa na mwandishi wa Jamhuri, alieleza
kuwa hamfahamu mtu anayeitwa Khalfan Kikwete na kwamba kampuni hiyo
inamilikiwa na familia yake (familia ya Simon) kwa asilimia 100.
Naye
Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam alieleza kuwa
hakuhusika na uuzwaji wa UDA na kwamba ulifanywa na viongozi
waliomtangulia. Alisema yuko tayari kuhojiwa na Taasisi ya Kupambana na
Kuzuia Rushwa (Takukuru) ili awaeleze ukweli.
“PCCB
wakija nitashukuru sana ili niweze kueleza ninachokijua, ila wakija hao
wanafiki wengine nitawafukuza maana mimi sipendi unafiki. Nataka
wakweli waje tu mimi nipo,” alisema Masaburi.
0 comments:
Post a Comment