MWENYEKITI
wa Bunge, Andrew Chenge leo ameahirisha bunge mara mbili kutokana na
mvutano ulioibuka baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuomba
bunge liahirishe kujadili hotuba ya rais na badala yake wajadili kuzuiwa
kwa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) kurusha matangazo ya moja
kwa moja.
Kabla ya kuahirishwa kwa bunge, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape
Nnauye aliwasilisha taarifa ya serikali kulieleza bunge kwamba,
serikali imesitisha huduma ya matangazo ya moja kwa moja kupitia TBC.
Kutokana
na taarifa hiyo, Zitto alisimama na kuliomba bunge kusitisha shughuli
za kuendelea kujadili hotuba ya rais ambayo ilianza kujadiliwa jana ili
kutoa fursa kujadiliwa hatua ya serikali kuzuia haki ya wananchi kupata
matangazao ya moja kwa moja kupitia televisheni hiyo.
Hata
hivyo, Chenge alianza kuonesha nia ya kutaka kuzima hoja ya Zitto
lakini wabunge wa upinzani kwa umoja wao waliungana na Zitto katika
kushikilia msimamo wa kujadiliwa suala la TBC kabla ya kuendelea na
mjadala wa hotuba ya rais.
Yalisikika
maneno kama ‘usituburuze, mtemi, hapa hakuna kuburuzana’ huku wabunge
wengine wakipiga kelele kuashiria kuunga mkono hoja ya Zitto.
Kutokana
na mvutano huo, Chenge alilazimika kuagiza kamati ya uongozi kukutana
ili kujadili taarifa hiyo na baadaye kuwasilisha kulichojadiliwa na
kamati hiyo.
“Naipa
kamati saa moja,” alisema Chenge jambo ambalo lilipokelewa kwa mikono
miwili na upinzani. Baada ya kauli hiyo mwenyekiti huyo aliahirisha
bunge kwa saa moja.
Hata
hivyo, baada ya bunge hilo kurejea tena baada ya kupita saa moja ,
Chenge aliahirisha tena bunge kwa kuwa, kamati ilikuwa haijamaliza
kujadili.
Wakati akizungumza bungeni wakati wa kuwasilisha kauli ya serikali Nape alisema, “naomba kutoa kauli ya serikali kuhusu TBC kutangaza moja kwa moja vikao vya majadiliano ya bunge.”
TBC
ilianza kurusha moja kwa moja matangazo ya vikao vya Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005. Kabla ya kuanza kurusha moja kwa
moja, TBC wakati huo televisheni ya taifa ilikuwa inarekodi matukio yote
ya bunge na kurusha usiku katika vipindi maalumu vilivyojulikana kama
bungeni leo kwa maana ya yaliyojiri ndani ya bunge kwa siku husika.
Hata hivyo Nape alisema “baada
ya kuanza kwa utaratibu wa kuanza kurusha matangazo moja kwa moja mwaka
2005, gharama za kufanya kazi hio zimekua zikipanda kwa kasi hadi
kufikia Sh. 4.2 bilioni kwa mwaka kwa maana ya mikutano minne ya bunge.
“Shirika
limekuwa likigharamia kwa sehemu kubwa matangazo hayo kwa kutumia
mapato yake yanayotokana na matangazo madogo madogo ya biashara,
ifahamike kuwa asilimia 75 ni vipindi vingi vinavyolenga kutoa elimu kwa
umma na asilimia 25 ni burudani.”
Nape
amesema, kutokana na hali hii, TBC imeona ni busara kubadilisha mfumo
wa utangazaji wa shughuli za bunge ili kukabiliana na kupanda kwa
gharama za uendeshaji.
Amesema
TBC imeona ni busara kuanzia mkutano huu wa bunge iwe inarusha baadhi
ya matangazo ya bunge moja kwa moja yaani ‘live’ ikiwa ni njia ya kubana
matumizi.
Amefafanua kuwa,
“chini ya utaratibu huu, TBC itahakikisha kuwa, baadhi ya matukio ya
matukio ya bunge yatarushwa moja kwa moja na mengine kurekodiwa na
kuandaliwa kipindi maalum kitakachoitwa leo katika bunge.
“Kipindi
hiki kitakua na mambo yote muhimu yaliyojiri ndani ya bunge kwa siku
husika. Kipindi hichi kitakuwa kinarushwa kuanzia saa nne usiku hadi saa
tano usiku.”
0 comments:
Post a Comment