Uchaguzi
wa kumpata meya wa Jiji la Dar es Salaam unatarajiwa kufanyika Jumamosi
katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee, Manispaa ya Ilala.
Hatua
hiyo inafuatia kukamilika kwa uchaguzi wa Mameya wa Manispaa za
Kinondoni, Ilala na Temeke. Kati ya hizo halmashauri mbili zilikwenda
kwa Ukawa na moja CCM.
Msemaji wa Halmashauri Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe alisema jana kuwa uchaguzi huo utafanyika kuanzia saa nne asubuhi.
Alisema wameshapokea maelekezo kutoka ngazi za juu yanayowataka kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika tarehe hiyo.
“Sasa hivi tunafanya maandalizi mbalimbali ikiwamo kutoa barua kwa wahusika,” alisema Makwembe.
Mwenyekiti
wa CCM wa mkoa huo, Ramadhan Madabida alisema chama chake kipo imara na
kimejiandaa vyema kushiriki uchaguzi na kuwataka wakazi Dar es Salaam
kusubiri matokeo. “...CCM hatuandikii mate, siku ya uchaguzi ikifika
wenyewe watajionea.”
Mkuu
wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alisema
Chadema na Ukawa kwa ujumla wamejipanga vizuri na kwamba wana uhakika
wataibuka kidedea kutokana mtaji wa madiwani walionao.
Alisema kinachotakiwa ni mamlaka husika kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa wa demokrasia ili mshindi apatikane kihalali.
“Tutahakikisha
tunakabiliana na mbinu zote chafu, zikiwamo za vitisho na rushwa kwa
madiwani wetu. Tunataka kuwaonyesha jinsi gani Ukawa ilijipanga kuongoza
Serikali,” alisema Makene.
Katika hatua nyingine; CCM Wilaya ya Ilala imepinga matokeo ya uchaguzi wa meya uliofanyika wiki iliyopita.
Katika
uchaguzi huo, madiwani wa CCM walisusia na kuwaachia Ukawa peke yao
ambapo, Charles Kuyeko (Chadema) alishinda kwa kura 31 na Omari
Kumbilamoto (CUF) akachaguliwa kuwa naibu wake kwa kura 31.
Mwenyekiti
wa CCM Wilaya ya Ilala, Asaa Simba alisema wapo kwenye mchakato wa
kumburuza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi mahakamani kwa
madai ya kutotendewa haki.
“Tumeanza
vikao vyetu na jopo la wanasheria wa chama ili kuangalia vifungu vya
kisheria na haki zilizokiukwa kisha twende mahakamani,” alisema Simba.
Alisema CCM haikushiriki uchaguzi huo kutokana na hatua ya wabunge walioteuliwa na Rais Magufuli kugomewa kupiga kura.
Alisema
sababu nyingine iliyowafanya wasishiriki uchaguzi huo ni hatua ya
wabunge wanane wa viti maalumu wakiwamo wanaotoka mikoa ya Zanzibar
kuzuiwa kupiga kura wakati walipewa barua za mialiko na mkurugenzi wa
manispaa hiyo.
Aliwataja
wabunge hao kuwa ni Amina Mollel, Stellah Ikupa, Mariam Ditopile,
Mwamtum Dau, Asha Juma, Martha Mlata, Anjelina Malembeka, Subira Mgalu
na kwamba Sophia Simba ndiye pekee aliyeruhusiwa kupiga kura.
0 comments:
Post a Comment