Thursday, 21 January 2016

#YALIYOJIRI>>>Tamko La Shirikisho La Vyama Vya Tiba Asili Tanzania (shivyatiata) Kuhusu Maelezo Ya Waziri Wa Afya Aliyoyatoa Tarehe 15/01/2016, Juu Ya Tiba Asili Natiba Mbadala.Fahamu zaidi hapa.

Ndugu waandishi wa Habari na ndugu wananchi, shirikisho la vyama vya Tiba Asili Tanzania (shivyatiata) ni chombo kinachosimamia vyama vyote vya Tiba Asili hapa Nchini pamoja na Waganga wote wa Tiba Asili na pia ndiyo msemaji wao kwa Serikali, Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa na kuhakikisha chombo hiki kinasimamia na kulinda maslahi yote ya Waganga wa Tiba Asili hapa nchini

Hivyo basi ,kutokana na maelezo yaliyotolewa na Waziri mwenye dhamana na mambo ya Afya mnamo hiyo tarehe 15/01/2016 shirikisho kwa kutambua dhamana tuliyonayo mbele ya Umma wa Waganga tunapenda kuwasilisha tamko letu kwenu nyinyi waandishi wa Habari na wanchi kwa ujumla ili muweze kuelewa yanayoendelea katika Tiba Asili hapa nchini.

Ndugu waandishi wa Habari, kwanza mtakumbuka kuwa mnamo tarehe 14/12/2015 Naibu waziri wa Afya maendeleo ya Jamii, jinsia, wazee na watoto Mhe. Dkt HAMISI KIGWANGALA (MB) alifanya ziara katika kituo cha Tiba Mbadala cha Tabibu anayejulikana kwa jina la Dr MWAKA. Baada ya ziara hiyo mengi yalizungumzwa na hata tamko la Wizara lililotolewa terehe 24/12/2015 lililohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa upande mmoja nalo lilichangia kuwepo kwa malumbano ya hapa na pale kutoka kwa watoa huduma wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, na wengine wakafikia hatua ya kupinga agizo hilo na kuitisha mgomo.
Ndugu waandishi wa Habari tunapenda mfahamu kuwa Wizara ya Afya katika kufikia kutoa tamko hilo la tarehe 24/12/2015 hawakushirikisha chombo chenye dhamana ya waganga ambacho ni shirikisho hili la vyama vya Tiba Asili Tanzania, Lakini kwa kutambua dhamana tuliyonayo kwa waganga wote wa Tiba Asili na kwa kutambua kuwa popote panapokuwa na mgogoro basi njia sahihi ni kukaa mezani kujadiliana ili hatimaye amani ipatikane.
Hivyo sisi Shirikisho tuliomba kikao na Mh. Waziri wa Afya ambacho kilifanyika tarehe 28/12/2015 na ambacho kilionesha nuru ya kufikia maelewano, Na kwa kuwa siku hiyo tarehe 28/12/2015 Waziri wa Afya Mhe. UMMY MWALIMU alitamka mbele ya vyombo vya habari kuwa yupo tayari kukaa kujadiliana na yeyote Yule ambaye amekwazwa na agizo la Wizara.
Hivyo sisi shirikisho tuliweza kukaa na wadau wa Tiba Asili na Tiba Mbadala ambao kimsingi ndiyo haswa walikwazika na agizo hilo la Wizara na hatimaye tarehe 31/12/2015 tulifanya kikao cha pamoja kati ya wadau hao, shirikisho, na Wizara ya Afya tukiongozwa na Uenyekiti wa Mhe. UMMY MWALIMU (MB) ambaye ndiye waziri mwenye dhamana na mambo ya Afya .
Ndugu waandishi wa Habari napenda ifahamike kuwa kikao hicho cha tarehe 31/12/2015 tulikubaliana kuwa wale wote wanaopeleka matangazo yao na vipindi kwenye Baraza kwa ajili ya kuhakikiwa basi Baraza liwaruhusu kuendelea na program yao hiyo na uhakiki wa Baraza usizidi siku tatu (3) kwa ujumla makubaliano yote ilikuwa ni utekelezaji wa sheria namba 23 ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya mwaka 2002 na kanuni zake na pia sheria nyinginezo za nchi na pia utekelezaji huu uwe wa pande zote, na mwisho Mhe Waziri alituhaidi kuwa tamko lingine la Serikali litatolewa tukiwa wote.
Lakini katika hali ya kushitua na kushangaza Mhe Waziri wa Afya ametoa tamko bila ya kutushirikisha sisi wadau wengine kama tulIvyokubaliana .
Hivyo tunaamini Waziri asingefanya hivyo kukiuka makubaliano isipokuwa ni kushauriwa vibaya na vyombo vya chini yake ambavyo vinadhammana ya kumshauri juu ya Tiba na tunaamini hivyo kwa kuwa viongozi wenye dhamana ya kumshauri walio chini yake wao ni wanataaluma ya Udaktari wa kisasa, Hivyo wameshindwa kumshauri Waziri vizuri kwa sababu wanapigania maslahi ya Taaluma yaona hawapo tayari kutoa ushirikiano wa dhati kwa Tiba Asili, lakini tunamuomba Mhe. Waziri kwa kuwa yeye ni mwanasheria basi aimome sheria namba 23 vizuri ili aweze kujiridhisha.
Tunaamini kuwa viongozi hao walio chini yake wangetumia nafasi na dhamana waliyo nayo kumshauri Mhe Waziri vizuri juu ya Tiba Asili bila kuweka mbele maslahi ya Taaluma yao, basi yote haya yasingetokea .
Ndugu waandishi wa Habari,  Tiba Asili imekuwepo hapa nchini kwa mika mingi kabla ya kuja tiba ya Kisasa ambayo kwa kadri siku zinavyozidi nayo inazidi kupoteza umaarufu wake na kuiacha Tiba Asili ikizidi kuchukua nafasi kubwa katika nchi yetu, Hivyo kitendo cha Tiba Asili na Sasa Tiba Mbadala kuzidi kuchukua nafasi kubwa kwa wananchi ambayo hivi sasa ni asilimia 70% mijini na asilimia 80% vijijini wanatumia Tiba Asili kitendo hicho kinawakera hao wanaoitwa madaktari wa kisasa na ndiyo maana maneno yamekuwa mengi kwa upande huu waTiba Asili na Tiba mbadala na kufikia hata hatua ya kutukejeri eti kwa nini tunavaa mavazi meupe wakati wa kutoa tiba?, kwa nini tunaitwa Madaktari kama wao?
 Na wengine hufikia kusema eti sisi waganga wa Tiba Asili na Tiba mbadala unaongoza kusababisha Vifo vya Wagonjwa kitu ambacho siyo kweli hata kidogo kwani Tiba Asili imeokoa na inazidi kuokoa maisha ya watu wengi mijini na vijijini, mfano mdogo katika Tiba Asili yapo magonjwa mengi yasiyoambukiza tunayatibu na pia tunaunga mifupa na waliovunjika hurejea katika hali yao ya kawaida ndani ya wiki mbili hadi mwezi mmoja kitu ambacho kwa Tiba ya Kisasa imekuwa ndoto kwao,

Lakini vilevile Tiba hiyo ya Kisasa ndiyo inaongoza kwa vifo vya watu wengi mijini na vijijini na ushaidi wa hilo ni uwepo wa mochwari karibu kila hospitali kwa ajili ya kuhifadhia maiti zitokanazo na watu waliokuwa ni wagonjwa na wakitibiwa katika Hospitali hizo na hao Madaktari bingwa wa Kisasa.
Ndugu waandishi wa Habari na ndugu wananchi, shirikisho la vyama vya Tiba Asili Tanzania tunapinga vikali matamshi yote yanayotolewa yakiwa yanalenga kuidhalilisha Tiba yetu ya Asili ambayo imekuwepo hapa nchini kwa miaka mingi na kwa sasa tunaiboresha na kuiendeleza ili iwe ya kisasa zaidi.
Hatupo tayari kuona watoa huduma wa Tiba Asili wananyanyaswa na kudhalilishwa ndani ya nchi yao, Hii ni nchi yetu sote.
Hivyo hakuna mwenye haki ya kujiona kuwa yeye na kundi lake ndiyo bora na wengine siyo bora, yeye ndiyo anahaki ya kuzungumzia mwili wa mtu na wengine hawana haki hiyo, yeye ndiyo ana haki ya kuvaa koti jeupe wakati wa kutoa Tiba na wengine haki yao ni kuvaa kaniki.
Kama kuna watu wapo tayari kuona hayo yanaendelea kutendeka sisi tunasema hatuko tayari na muda wote hatutokuwa tayari.
Hivyo katika hili tamko lililotolewa tarehe 15/01/2016 na Mhe Waziri wa Afya tunabainisha mambo gani tunayaunga mkono na mambo gani hatuyaungi mkono
MAMBO TUNAYOYAUNGA MKONO
  1. Tunaunga mkono Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kuongezwa watumishi wa kutosha lakini wawe na moyo wa kuipenda Tiba Asili na Tiba mbadala
  2. Tunaunga mkono kuwepo mpango mkakati kwa muda mrefu kuwezesha kufanikisha uboreshaji wa Huduma wa Tiba Asili na Tiba mbadala lakini mpango huo uwe wa vitendo zaidi.
  3. Tunaunga mkono watoa huduma wote, vituo vyote vya kutolea huduma, dawa na vifaa tiba vinasajiliwa .
  4. Tunaunga mkono mwongozo wa mafunzo kwa watoa huduma wote nchini kuhusu namna ya kuweka kumbukumbu za wagonjwa , kutoa rufaa kwa wagonjwa (lakini rufaa hizo ziwe kwa pande zote siyo waganga tu kupeleka wagonjwa mahospitalini na mahospitali nayo yalete wagonjwa wao kwa waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala)
  5. Pia tunaunga mkono kuwepo kwa mawasiliano kati ya Wizara Afya na Wizara zinazohusika na mambo ya Habari, OFISI YA RAIS Tamisemi, na Taasisi za utafiti
MAMBO AMBAYO HATUYAUNGI MKONO
  1. Hatuungi mkono kuondolewa kanuni inayoruhusu matangazo kwa idhini ya Baraza isipokuwa tunataka sheria iachwe kama ilivyo juu ya utoaji wa matangazo .
  2. Hatuungi mkono kuongezwa adhabu kwa sababu hata iliyopo haijawahi kutumika kwa wakosaji 
  3. Hatuungi mkono kuweka ukomo wa usajili mijini na vijiji kwa sababu tangu usajili uzinduliwe ni miaka mitano sasa na waganga waliosajiliwa hawazidi elfu kumi na moja (11,000), Hivyo siyo kazi rahisi kusajili waganga elfu sitini na nne(64,000) kwa muda wa miezi mitatu na sita, ikiwa wapo watu wamejaza fomu za Baraza tangu mwaka 2011 na walilipia Ada za usajili Banki lakini hadi leo hawajapata vyeti, kwa hiyo hata hatua ya kuwazuia wasitoe huduma hilo haliwezekani.
  4. Hatuungi mkono kuzuia kuuza dawa au kugawa dawa eti hadi iwe imesajiliwa na Baraza, kupimwa na maabara ya mkemia mkuu wa serikali na kupewa kibali na TFDA hilo halikubaliki kwa sababu tunaamini kuwa TFDA ni mmoja ya wanaosababisha migogoro ya Waganga ikiwemo kutoa vibali vya waganga kutangaza katika Radio na Televisheni na hali hawaruhusiwi kutoa vibali hivyo lakini Wizara ya Afya wameshindwa kuikemea TFDA, Tunataka utaratibu wa kupima dawa, kusajili katika Baraza uende sambamba na uuzaji na ugawaji wa dawa hizo kwa wagonjwa .
  5. Hatuungi mkono agizo la kusajili vifaa tiba TFDA kwani agizo hilo siyo la kisayansi na halitekelezeki kwa mazingira yaliyopo hapa nchini ambayo hivi sasa wapo watu wengi wananunua na kutumia vifaa tiba kwa ajili ya kujiangalia Afya zao kwa hiyo siyo kazi rahisi kwa mtu binafsi kwenda kusajili mashine ya Glukosi TFDA tunataka waachwe wavitumie kwa kuwa wao ndiyo wanavitumia na kuviamini.
  6. Hatuungi mkono kuzuia matangazo ya aina yoyote yanayohusu Tiba Asili kwa sababu sheria inaelezea utaratibu wa kutangaza , na pia tunaomba ifahamike kuwa matangazo yanayohusu Tiba Asili hayamuthiri mwananchi yeyote ikilinganishwa matangazo ya sigara na vilevi vingine lakini Wizara ya Afya ipo kimya juu ya matangazo hayo na kuacha watu wengi wakiangamia kwa kutumia vitu hivyo. Kama hoja ni Tiba isitangazwe kwa Dunia ya sasa haiwezekani watu ni wengi na vifaa vya kutangazia vipo, zamani watu walikuwa wachache na hakukuwa na vifaa vya kutangazia, isitoshe hata Ibada zinatangazwa kwanza ndiyo utaona watu wanajaa makanisani na misikitini kwa hiyo kusema Tiba isitangazwe haikubaliki hata kidogojambo la msingi ni kuboresha utaratibu iliopo unaohusu matangazo na siyo kuuondoa .
Uganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala siyo jambo la kuhujumu uchumi wala madawa ya Tiba Asili si madawa ya kulevya . Na pia kuwazuia watoa huduma kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara kuhusu Tiba Asili na Tiba Mbadala nalo halikubaliki hata kidogo, Huo ni uvunjifu wa katiba na ni kinyume cha haki za Binadamu na pia itakuwa ni kuingilia Taaluma ya Mtu, isipokuwa zuio liwe kwa mtu ambaye si Mganga.
Hivyo basi kutokana na hayo tuliyoyaeleza tunaamini kuwa sisi waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala tunahujumiwa na tunaamini kabisa wapo watu hawaitakii mema tiba yetu hii, hivyo tunataka mambo yafuatayo yatekelezwe:-
  1. Viongozi wote wenye dhamana ya kumshauri Waziri juu ya Tiba kwa kuwa wameshindwa kumshauri vema na wameegeme kupendelea Taaluma yaoTunaomba mamlaka ya juu iingilie swala hili ili haki itendeke
  2. Tiba Asili iundiwe Wizara yake kwa sababu madaktari wa kisasa sisi tunawapenda lakini wao hawatupendi wanaona Wizara ya Afya ni ya kwao peke yao.
  3. Ili tuwe na Imani na Wizara ya Afya tunataka tuwe na Mganga mkuu wetu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala wa serikali kuliko kuwa na hawa wa kawaida ambao kazi yao kubwa ni kupendelea Taaluma zao.
  4. Kuanzia sasa Waganga wote wasajiliwe na shirikisho kwa kuwa ndiyo linaweza kuwatambua na kuwafuatilia kwa karibu utoaji wao wa huduma na Baraza libaki na kazi ya kuthibitisha vyeti vyao tu.
  5. Tunataka heshima ya Tiba Asili ienziwe na siyo kudharauliwa.
  6. Tunataka waziri mwenye dhamana na Afya awaeleze Watanzania ni watu wangapi wanakufa kwa siku katika hospitali za serikali na za Binafsi ambazo zina hao wanaoitwa Madaktari bingwa.
  7. Mamlaka ya juu ya Wizara ya Afya kwa maana ya Ofisi ya Waziri mkuu tunaomba iingilie kati swala hili, ikae na sisi wadau wa Tiba Asili ili ukweli ujulikane na muafaka upatikane tunaamini katika majadiliano, na tunaimani na Serikali yetu inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt. JOHN POMBE MAGUFULI.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza
ABDULRAHMAN M. LUTENGA
Mwenyekiti wa Taifa wa Shirikisho la vyama vya Tiba Asili Tanzania
Tarehe 16/01/2016

0 comments:

Post a Comment