KANISA
la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN) lililopo jijini
Mwanza, limemtimua rasmi Askofu kanisa hilo, Boniface Kwangu, kutokana
na ubadhilifu wa zaidi ya Sh. 600 milioni.
Askofu
huyo ni wa pili kutimuliwa na uongozi wa kanisa hilo baada ya mwaka
2007 aliyekuwa Askofu wa dayosisi hiyo, John Changae na yeye kufukuzwa
kutokana na matumizi mabaya ya madaraka kitendo ambacho kinaonesha
taswira mbaya kwenye kanisa hilo.
Pia
Askofu Kwangu aliyedumu kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka
minane, katika uongozi wake alishawahi kutuhumiwa na waumini wake kuwa
anajihusisha na dini ya Freemasons huku wengine walikuwa wakimtuhumu
kwamba anatumia nguvu za giza.
Askofu
Kwangu na wenzake wanne wanatuhumiwa na kanisa hilo kwa ubadhilifu wa
zaidi ya Sh. 600 milioni pamoja na kuendesha kanisa hilo bila kufuata
kanuni na taratibu za kanisa hilo kitendo ambacho kimesababisha
kutimuliwa kwake.
Askofu
Kwangu, anatuhumiwa na upotevu wa Sh. 500 milioni ya shule ya kimataifa
ya Isamilo, kuuza gari la dayosisi hiyo, kufukuza wafanyakazi wa kanisa
hilo na kusababisha wadaiwe Sh. 60 milioni, kujipatia kiasi cha zaidi
ya Sh. 15 milioni kutoka kwa Mhasibu wa kanisa, Sam Wisa, bila kibali.
Akisoma
tamko la kumfukuza kazi, Mwenyekiti wa Nyumba ya Wadumu kutoka DVN,
Andrew Kashilimu, amesema askofu huyo ameisababishia hasara kanisa hilo
zaidi ya Sh. 600 milioni, kutokana na kufanya kazi bila kufuata kanuni
na taratibu.
Amesema
kuwa askofu Kwangu amekiuka viapo vya uaskofu, katiba ya jimbo, katiba
ya DVN na amekiuka maadili na kanuni, kuendekeza matabaka ndani ya
wahudumu na waumini, kutoa ajira ndani ya DVN kinyume na taratibu za
kanisa.
Amesema
katika kikao kilichoketi Septemba 1 mwaka jana, kilithibitisha mambo
hayo na kukubaliana kwamba Askofu huyo ajiuzulu kwa afya ya kanisa la
Mungu lakini alikaidi maagizo hayo mpaka kutoka kwa tamko hilo.
“Askofu
(Boniphace Kwangu) ametumia vibaya madaraka yake na alikuwa anatumia
vibaya mali na fedha za kanisa, kwa hali hiyo tusingeweza kuwa na
kiongozi wa namna hiyo,” amesema Kashilimu.
Mmoja
wa waumini ambaye alikumbwa na fagio la Askofu, Kwangu, Edwar Kibiti,
amesema kwamba kutimuliwa kwa kiongozi huyo wa kiroho katika kanisa hilo
kutasaidia kurudisha matumaini kwa waumini walio wengi.
Kibiti
ambaye pia ni Mchungaji amesema kuwa walipokuwa wakijaribu kuhoji
sababu za Askofu Kwangu kuuza mali za kanisa ikiwamo gari alilochangiwa
na waumini alikuwa akiwafukuza watu waliotaka kufahamu suala hilo.
“Tulipokuwa
tunahoji matumizi ya mali za kanisa tulichokuwa tukiambulia ni kwenda
polisi na wengine wafukuzwa, huyu (Askofu Boniphace Kwangu) alikuwa
anafanya kazi kwa majungu na mpaka anaondoka alishafukuza wachungaji
19,” amesema Kibiti.
Amesema
kuwa baada ya askofu huyo kuona wachungaji wazawa wanaanza kumfuatilia
alianza kutafuta wachungaji wengine kutoka nchi mbalimbali hususani
kutoka Rwanda, ili kuficha maovu yake anayoyafanya.
Mmoja
wa Waumini, Joycelyn Juma, amesema kilichomgharimu askofu huyo ni
upungufu wa mambo ya kiuongozi ambayo yamechangia kusababisha kuwepo kwa
mwanya wa wizi wa mali na fedha za kanisa hilo.
“Kiufupi
nimefurahi sana kwa sababu mambo ya ufisadi ama wizi wa fedha
haviendani na mambo ya Mungu na nimefurahi kuona suala hili limefikia
mwisho na sasa tutakuwa na amani,” amesema Juma.
Sanjali
na kufukuzwa kazi ya Uaskofu DVN, pia uongozi wa kanisa hilo
limemfungulia kesi Askofu Kwangu na wenzake wanne, Katibu wa Bodi, James
Mtaritinya, Mhasibu wa Shule ya Isamilo, Sam Wisa, Samson Maganga na
John Magawa.
Kesi iliyofunguli ni Januari 10 mwaka huu, Mw/Rb/265/2016 ambalo ni jalada la uchunguzi kwa watuhumiwa.
0 comments:
Post a Comment