TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU ZOEZI LA KUHAMISHA WAKAZI WA MABONDENI KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM
Utangulizi
Nchi
yetu ina kingo za mito na mabonde na maeneo mengi hatarishi ambamo watu
wanaishi kinyume cha sheria, huku wakiharibu mazingira na kuhatarisha
maisha yao. Kutokana na uhaba wa makazi, hali ni mbaya zaidi katika
mabonde ya Jiji la Dar es Salaam, hasa bonde la Mto Msimbazi.
Serikali
za awamu zote, zimekuwa zikifanya jitihada za kuwaondoa wakazi wa
maeneo ya mabondeni wanaoishi katika maeneo hayo kinyume cha sheria
lakini mafanikio yamekuwa si ya kuridhisha.
Serikali
ya Awamu ya Tano, ambayo moja ya misingi yake mikuu ni utii wa sheria
za nchi, imeanza jitihada za kuwaondoa wakazi hawa.
Tuliamua
kuanza na Bonde la Mto Msimbazi kwasababu ndiko kwenye watu wengi na
athari kubwa.Sababu zetu kuu za kufanya zoezi hili ni kusafisha mabonde
na mito katika jiji la Dar es Salaam na mazingira yanayozunguka ni:-
Kunusuru maisha ya wananchi
wanaoishi katika mazingira hatarishi. Eneo la Bonde la Mto Msimbazi
lilitangazwa kuwa ni eneo hatarishi kuishi binadamu tangu mwaka 1949 na
baadaye 1979.
Kupanua uwezo wa mito ya Dar es Salaam
ili kupitisha maji ya mvua kwa kasi kubwa, hivyo kupunguza uwezekano wa
kutokea mafuriko na maafa wakati wa mvua nyingi;Kuzuia milipuko ya
magonjwa, hasa ya kipindupindu, hasa wakati wa mvua;
Kuzuia eneo hilo kuendelea kutumika kama maficho ya wahalifu na uhalifu;
Kutoa nafasi kwa Serikali kuandaa na kuendeleza eneo hilo kwa mujibu wa sheria za nchi na mipango miji;
Utaratibu wa Zoezi
Kabla
ya nyumba kubomolewa, taasisi hizi zinashirikiana kuhakiki iwapo nyumba
anayokaa mkazi ina nyaraka za umiliki na vibali vya ujenzi na iwapo
nyaraka hizo zina uhalali wowote.
Nyumba
ambazo zimethibitika kuwepo katika maeneo yasiyostahili ndio zinawekwa
alama X kuashiria kwamba wakazi wanapaswa kuhama au kubomoa. Baada ya
hapo, mkazi hupewa muda wa kubomoa na kuhama mwenyewe.
Kutokana na utaratibu huu, sehemu kubwa ya nyumba zinazobomolewa ni zile ambazo watu wamekwishaamua kubomoa wenyewe.
Baada
ya hapo, alama huwekwa kuonyesha mpaka wa bonde. Katika zoezi hili,
imebainika kwamba sehemu kubwa ya wakazi wa maeneo ya mabondeni ni
wapangaji huku wamiliki wakikaa sehemu nyingine salama.
Serikali pia imeweka Dawati la Malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Tathmini ya Zoezi
Jana,
terehe 7 Januari 2016, Mawaziri watatu (Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI; na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais; pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili
na Utalii), walifanya mkutano wa kutathmini zoezi la kuhamisha wakazi wa
mabondeni katika Jiji la Dar es Salaam.
Mkutano
huo ulipokea ripoti ya timu ya wataalam wa Wizara mbalimbali,
inayoongozwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira,
ambayo, pamoja na mambo mengine ilibainisha kwamba sehemu kubwa ya
kubaini makazi yaliyojengwa kinyume cha Sheria katika Bonde la Mto
Msimbazi imekamilika.
Ripoti
ilieleza kwamba, hadi sasa, wananchi katika nyumba 774 wamehama na
nyumba hizo kubomolewa. Ilielezwa pia kwamba kabla ya mkazi kuombwa
kuhama, uhakiki kuhusu uhalali wa makazi anayoishi hufanywa.
Kutokana
na uhakiki huo, jumla ya wakazi 20 walikuwa na hati halali za makazi na
wakazi 119 walikuwa na leseni za makazi za muda mfupi.
Hawa watu hawakuhamishwa. Mawaziri walipokea maelezo kuhusu changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi hilo.
Baada ya tafakuri na mjadala, Mawaziri hao walitoka na msimamo ufuatao, kama uamuzi wa Serikali: -
1.Zoezi
la kuwaondoa wananchi waishio katika bonde la Mto Msimbazi (eneo
hatarishi) litaendelea kwa utaratibu ambao hautaleta mateso na usumbufu
kwa wananchi;
2.Katika awamu hii, zoezi litajikita katika Bonde la Mto Msimbazi tu.
3.Kwa
wakati huu, watakaohitajika kuhama ni wale tu ambao makazi yao yamo
NDANI kabisa ya bonde, kwenye miteremko ya kuingia bondeni na kwenye
KINGO za mto;
4.Wale
watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za umma,
zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo,
hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za kujenga. Na watumishi wa
umma waliowamilikisha maeneo hayo watachukuliwa hatua za kinidhamu na
kisheria;
5.Serikali, ndani ya siku tatu zijazo, itaanza zoezi la kuzoa kifusi na kusafisha maeneo ambapo ubomoaji umefanyika.
6.Serikali
itaheshimu amri za mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya
wakazi wa mabondeni lakini pia itafuatilia kesi hizi ziishe haraka ili
taratibu zinazofuatia zifanyike;
7.Serikali
itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake wanaoendesha zoezi hili
kinyume na misingi ya sheria zinazotekelezwa, na kinyume na misingi ya
haki na uwazi, ikiwemo wanaoweka alama za X zaidi ya mita zilizowekwa
kisheria. Limeanzishwa dawati la malalamiko katika Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kupokea malalamiko au maswali
kuhusu zoezi hili.
8.Nyumba
na majengo ya miaka mingi, yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa
kwa Sheria zinazotekelezwa kwa zoezi hili, hayatabomolewa isipokuwa tu
pale maisha ya wakazi yapo hatarini. Wanaoishi katika makazi hayo
watapewa miongozo ya hatua za kuhifadhi mazingira na kujiokoa na maafa;
9.Serikali
haina dhamira ya kubomoa mahoteli makubwa ya siku nyingi yaliyo karibu
na fukwe katika maeneo ya Masaki. Wamiliki wa mahoteli haya watapewa
masharti na miongozo ya kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria.
10.Serikali
inaweka uratibu wa karibu zaidi miongoni mwa taasisi zake ili hatua za
utekelezaji wa sheria za nchi zisiwe chanzo cha taharuki katika jamii.
11.Serikali
haina dhamira ya kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha kuhama katika
makazi yao bila sababu za msingi. Lakini pia Serikali haiwezi kuruhusu
wananchi waendelee kukaa katika maeneo ambayo ikinyesha mvua kubwa
maisha yao yapo hatarini.
Itakumbukwa
kwamba katika mafuriko ya mwaka 2011, wananchi 49 waishio mabondeni
walipoteza maisha. Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Hali ya Hewa,
mwaka huu zinatarajiwa kunyesha mvua kubwa kuliko zilizowahi kutokea
katika miaka ya hivi karibuni.
12.
Serikali inafuatilia kwa karibu kwa mamlaka za Serikali za Mitaa juu ya
taarifa za wananchi wanaohitaji msaada maalum wa kibinadamu.
Suala la Mchungaji Getrude Rwakatare
Mkutano
ulipokea taarifa kuhusu suala linaloongelewa sana la nyumba ya
Mchungaji Rwakatare. Ilielezwa kwamba Mchungaji Rwakatare amejenga
nyumba yake pahali ambapo amezuia mtiririko wa mto kwa kujaza kifusi ili
kupata eneo zaidi katika eneo la miti ya mikoko, kinyume kabisa na
Sheria tatu muhimu.
Pia
ilielezwa kwamba tangu wakati ujenzi unaanza jitihada za kumsimamisha
zilifanyika na mamlaka za Serikali za Mitaa lakini ikashindikana
kutokana na sababu mbalimbali. Pale Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira lilipoingilia kati na kutaka kuibomoa nyumba
hiyo, Baraza lilishtakiwa mahakamani.
Wakati
kesi inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza, yeye
mwenyewe bila kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, mnamo tarehe 11 Mei
2015, aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba
ya Baraza ya kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali, kwa niaba ya
Baraza, kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.
Makubaliano
hayo yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu tarehe 13 Mei 2015.
Mwanasheria huyo alificha makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba
2015, yalipogundulika na mtumishi mwingine wa Baraza. Mkutano ulielezwa
kwamba Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kufuata taratibu
zote, alishaagiza kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa
mwanasheria huyo.
Mwanasheria huyo alifukuzwa kazi siku ya juzi tarehe 6 Januari 2016 na taarifa zake zimekwishafikishwa TAKUKURU.
Vilevile,
Ofisi ya Makamu wa Rais, iliiagiza Baraza kufungua shauri mahakamani la
kuomba “makubaliano” kati yake na Mchungaji Rwakatare yawekwe pembeni
kwasababu yalipatikana na njia ya udanganyifu. Shauri hilo lilifunguliwa
tarehe 29 Disemba 2015.
Kuhusu Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Kasi (DART)
Mkutano
pia ulijulishwa kuhusu hoja inayozungumzwa kwamba wananchi wanaondolewa
katika maeneo ya kuishi mabondeni lakini mradi wa DART umeachwa.
Mkutano
ulielezwa kwamba Sheria ya Mazingira (kifungu 57 (2)) inatoa nafasi ya
kutolewa ruhusa kwa miradi/shughuli zenye maslahi ya taifa kufanyika
katika maeneo ya mabondeni, na kwamba Waziri mwenye dhamana ya mazingira
anaruhusiwa kutoa miongozo ya namna ya shughuli hizo zinavyoweza
kufanyika bila kuathiri mazingira.
Mradi
wa DART ulipata kibali hicho na una mkataba na Baraza la Mazingira
kuhusu hatua za hifadhi ya mazingira zinazopaswa kutekelezwa katika
mradi huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
08.01.2016
0 comments:
Post a Comment