Watanzania
leo wanaanza kufaidi elimu bure kufuatia kufunguliwa kwa shule za umma
huku Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce
Ndalichako, akisema fedha zimeshafika kwa kila shule.
Aidha, Prof. Ndalichako amewataka wamiliki wa shule binafsi kujitathmini.
Itakumbukwa
kuwa serikali ilipoanzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi na
Sekonari mwaka 2000, lengo lilikuwa ni kutoa ruzuku ya Sh.10,000 kwa
kila mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh. 25,000 kwa kila mwanafunzi wa
sekondari kwa mwaka.
Ruzuku
hiyo inalenga kugharimia ununuzi wa vitabu vya kiada na ziada, vifaa
vya kufundishia zikiwamo chaki, madaftari, kalamu za risasi na wino,
karatasi za kufanyia mitihani, ukarabati miundombinu ya shule na shughui
za utawala.
Juzi,
Prof. Ndalichako alisema kuwa fedha za ruzuku kwa wanafunzi shule za
msingi na sekondari, zimeshapelekwa, lengo likiwa ni kuhakikisha leo
wanafunzi wanaanza masomo.
“Fedha hizi zitakuwa zikitolewa kwa awamu, kwa hiyo zilizokwenda ni awamu ya kwanza tu,” Alisema Profesa Ndalichako
Prof.
Ndalichako alisema ili kuhakikisha fedha zote zinazotolewa zinafika kwa
walengwa, watashirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi), kuhakikisha zinawafikia walengwa.
Alisema moja ya njia ya kufikia lengo hilo ni kutoa fedha hizo kwa awamu na kuhimiza uaminifu kwa watu wote wanaohusika.
Ada Elekezi Kwa Shule Binafsi
Akizungumzia
ada elekezi, alisema suala hilo ameona ni vyema lifanyiwe utafiti kwa
kila shule kufafanua matumizi ya fedha wanazotoza na kuwa na baada ya
kukubaliana ada elekezi, watakaokiuka watakabidhiwa kwa Mamlaka ya
Mapato (TRA), ili watozwe kodi.
“Hili
suala nimelikuta na nikaona ni vyema tufanye utafiti kidogo. Sasa hivi
shule nyingi tayari zina viwango vya ada na vina tofauti kubwa tu. Kwa
kuanzia, nimeona tuanze na ada zilizopo, tayari nimeshaelekeza na kazi
imeanza kwa kutaka wamiliki wa shule watoe `justification’ (hoja za
kuhalalisha) ada wanazotoza,” alisema na kuongeza:
“Nimeona
kuna umuhimu wa kushirikisha hawa watu na kuwasikiliza, ndiyo maana
tukasema kwanza wao watupatie hayo maelezo. Mtu aseme labda anatoza Sh.
milioni tano, atuambie ana walimu wangapi, mishahara yao Sh. ngapi?
Gharama za umeme ni Sh. ngapi?
"Akisema
gharama za chakula na sisi tunazijua, tutaangalia hata kama anawapa
watoto soseji, tutaangalia bei na kadhalika, tunachotaka kwanza tutafute
uhalisia wa hizo ada.
“Najua
kuna baadhi ya maeneo tutakosa uhalisia maana mwingine anatoza bei ya
umeme labda kila mwanafunzi Sh. 20,000, kama ana wanafunzi 500, jumla
yake itakuwa Sh. ngapi? Tutamwambia atupe bili ya umeme tuthibitishe,” alisema Pro. Ndalichako.
Alisema
wameamua kufanya hivyo kwa kuwa shule binafsi zina mazingira tofauti na
hivyo ni vigumu kuwa na ada elekezi moja ambayo kweli inatekelezeka.
“Ada
elezi haiwezi kuwa sawa kwa sababu shule zina viwango tofauti na walimu
aina tofauti. Hata maeneo zilipo, ni tofauti, pia kuna huduma tofauti
zinazotolewa na shule hizi.
Kila
shule ikitoa mchanganuo, tujua kilichopo, tukiwa na data (takwimu)
itatusaidia kujua mengi na sisi kujipanga vizuri, hata vyakula
wanavyotoa tutaviangalia na kuvihakiki, usije kutoza Sh.15,000 kwa
chakula kwa siku halafu ukampa mtoto ugali na maharage,” alisema.
Alisema
pamoja na mambo mengine, vitu hivyo vitathibitishwa na wakaguzi wa
shule na pale inapobidi wazazi watashirikishwa ili kupata uhalisia.
“Tutachukua
muda, lakini tutakuja na majibu ambayo Watanzania wote watakubali kwa
sababu sasa hivi wapo ambao hawapo na sisi wizara, hatutaki kumwambia
mtu anayetoa kompyuta, na vitu vingine muhimu kwa mwanafunzi aache.
"Lazima
tushirikiane nao ili hata kwenye utekelezaji tufanikiwe, ambacho
hatutaki ni shule kutumia sana wanafunzi kama sehemu ya kipato na
tukiweka ada elekezi wale watakaotoza zaidi, tutawapeleka TRA wawatoze
kodi kwa sababu hawa wanafanya biashara, wanazalisha,” alisema Prof. Ndalichako.
0 comments:
Post a Comment