NAIBU
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi
Kigwangalla amesema Serikali imekamilisha mapendekezo ya uundwaji wa
Sheria ya Wazee ambayo yatawasilishwa katika mkutano wa Bunge wa
Septemba.
Dk.
Kigwangalla aliyasema hayo jana (Ijumaa, Aprili 29, 2016) wakati akitoa
ufafanuzi kwa Viongozi wa Mtandao wa Wazee waliomtembelea Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa ofisini kwake mjini Dodoma.
Dk.
Kigwangalla alisema kuwepo kwa Sheria ya Wazee kutawezesha mambo
mbalimbali yanayohusu wazee kutekelezwa kwa mujibu wa sheria hiyo
likiwemo suala la pensheni.
“Mimi
pamoja na Waziri wangu, Ummy Mwalimu baada ya kupewa jukumu la kuongoza
wizara tuliunda kikundi cha wazee kwa ajili ya kuamua mambo makubwa
mawili ambayo tutayatekeleza likiwemo la pensheni kwa wazee wote,” alisema.
Naibu
Waziri huyo alisema suala jingine ambalo wamepanga kulitekeleza ni
utoaji wa huduma ya bure kwa wazee, ambapo watawapatia bima ya afya ili
wasiendelee kusumbuka.
Kwa
upande wake Waziri Mkuu aliwahakikishia wazee hao kwamba Serikali
inawatambua na ndiyo sababu ya waliamua wawe na sehemu ya kufikishia
malalamiko yao ambayo ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto .
Kuhusu
ombi la wazee hao kwa Rais Dk. John Magufuli la kuwa na uwakilishi
Bungeni kwa kupitia nafasi zake 10 za uteuzi, Waziri Mkuu alisema
amelipokea na atalifikisha kwa Mhe. Rais.
Pia
amewataka wapanue taasisi yao na kuimarisha mtandao uweze kujulikana na
wazee wengi zaidi, wawe na viongozi kuanzia ngazi za vijiji ambapo
Serikali ipo tayari kushirikiana nao kwa karibu.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na utoaji wa huduma
za afya kwa wazee katika hospitali mbalimbali alizotembelea na kukuta
yameanzishwa madirisha maalumu ya kuhudumia.
Akizungumzia
kuhusu suala la wazee kupewa elimu ya mapambano dhidi ya UKIMWI
aliwataka waandaaji wa matamasha na semina za mafunzo hayo kujumuisha
watu wote wakiwemo wazee.
Naye
Mwenyekiti wa mtandao huo , Bw. Sebastian Bulegi alisema lengo la
kumtembelea Waziri Mkuu ni kumuomba awafikishie shukurani zao kwa Rais
Dk Magufuli kwa kuwapatia wizara maalumu inayoshughulikia masuala yao.
“Vile
vile shukurani hizi tufikishie kwa mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli
kwa kufanya wazee kuwa agenda yake ya kwanza na tayari ameshatembelea
makazi ya Nunge Kigamboni (Dar es Salaam) na Bukumbi (Mwanza),”alisema.
Mwenyekiti
huyo ambaye aliambatana na wajumbe wanane wa mtandao huo unaoundwa na
Asasi 26 za wazee katika ngazi za wilaya na mkoa kutoka mikoa ya Kigoma,
Tanga, Arusha, Mwanza, Lindi na Dodoma, aliiomba Serikali isimamie
kutokomeza mauaji ya wazee.
Ombi
jingine alilolitoa kwa Serikali ni utekelezwaji wa Sera ya Wazee ya
mwaka 2003, Sera ya Matibabu bure kwa wazee, mafunzo ya kupambana na
UKIMWI pamoja na uwakilishi katika ngazi za kutoa maamuzi.
Pia
wazee hao wamemhakikishia Waziri Mkuu kwamba wamekubali ombi
linalotolewa na viongozi wakuu wa nchi la kuwataka wawaombee ili waweze
kutekeleza majukumu yao ipasavyo, baada ya kuridhishwa na utendaji kazi
wa Serikali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980, DODOMA.
JUMAMOSI, APRILI 30, 2016.
0 comments:
Post a Comment