Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kiama kwa
wafanyabiashara wa vifaa vya mawasiliano, kuacha kuwahadaa wananchi kwa
kutoa punguzo ili kuwashawishi kununua simu bandia na kutishia kuwafunga
miaka 10 jela, faini ya Sh30 milioni au vyote kwa pamoja
watakaobainika.
Hatua hiyo imekuja wakati mamlaka hiyo ikiwa
katika hatua ya kutekeleza mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa
vifaa vya mawasiliano vya mkononi, huku ikitarajia kuzima simu feki
ifikapo Juni 16.
Akizungumza na vyombo vya habari jana, Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA, Mhandisi James Kiraba alisema kuna
wafanyabiashara wajanja wanaobadilisha namba za utambulisho za vifaa vya
elektroniki (IMEI) ili kuwahadaa wateja kuwa simu zao siyo feki.
Kwa ujanja huo, namba ya utambulisho inakuwa inatumika na simu zaidi ya moja na kutambulika na mfumo licha ya kuwa ni feki.
Pamoja
na kuonekana ni halisi kwa kipindi wanachozinunua, alisema simu hizo
zinazobadilishwa IMEI nazo zitazimwa Juni 16 kwa kuwa ni feki.
“Mamlaka
inawakumbusha wauzaji wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi kuwa ni kosa
kubadilisha namba tambulishi za vifaa vya simu za mikononi (mobile
devices), kwani adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka 10 au faini
isiyopungua Sh30 milioni au vyote kwa pamoja,”alisema.
Alisema
kumekuwa na udanganyifu kwa baadhi ya wauzaji wa simu kwa kutoa punguzo
kwa wananchi ili kuwashawishi kuzinunua simu bandia kwa bei nafuu.
Kiraba
alisema wananchi wanapaswa kuwa makini na hilo, huku wakihakikisha kuwa
simu zao zimehakikiwa ili kuzuia usumbufu wa aina yoyote, utakaoweza
kujitokeza wakati kipindi cha mpito kitakapomalizika.
Alisema
idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (bandia)
zimeendelea kupungua kutoka asilimia 30 Desemba mwaka jana hadi kufikia
asilimia 13 Machi.
Alisema uchambuzi wa Februari ulionyesha
idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa
na asilimia tatu, vilevile idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa
zilikuwa sawa na asilimia 18 huku simu halisi zilikuwa sawa na asilimia
79.
“Uchambuzi wa Machi unaonyesha idadi ya namba tambulishi
ambazo hazina viwango zilikuwa sawa na asilimia nne, huku idadi ya namba
tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na asilimia 13, uchambuzi
huu unahusisha makampuni yote ya simu nchini,” alisema.
0 comments:
Post a Comment