Aliyekuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) Ephraimu Mgawe
(Kulia) na Makamu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Hamadi Koshuma
*****
Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Ephraim Mgawe
na aliyekuwa Naibu wake, Hamad Koshuma wana kesi ya kujibu ya matumizi
mabaya ya madaraka, imefahamika.
Mgawe na mwenzake wanakabiliwa
na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kutumia
madaraka yao vibaya kwa kutoa zabuni kwa kampuni ya China ya
Communication Construction Company Limited kwa ajili ya ujenzi wa magati
katika Bandari ya Dar es Salaam.
Jana mahakama hiyo katika
uamuzi wake baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka, iliwaona
washtakiwa hao kuwa wana kesi ya kujibu kwa mashtaka yanayaowakabili,
hivyo watapanda kizimbani kujitetea, Mei 16 mwaka huu.
Akitoa
uamuzi huo, Hakimu Mkazi Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo, alisema
kwamba ameridhika kuwa upande wa mashtaka umeweza kujenga kesi dhidi ya
washtakiwa hao na kuwa wana kesi ya kujibu.
“Baada ya kupitia
ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka pamoja na vielelezo,
nimeridhika kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu, hivyo wanatakiwa kutoa
utetezi wao,” alisema hakimu Mkeha.
Baada uamuzi huo, Mgawe
aliieleza mahakama kuwa anatarajia kuita mashahidi tisa kumtetea
mahakamani hapo, huku Koshuma akisema kuwa yeye atajitetea mwenyewe na
kwamba hatakuwa na shahidi mwingine.
Mgawe na Koshuma wanadaiwa
kula njama na kutoa zabuni tata kwa kampuni hiyo kwa ajili ya kujenga
maghati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa gharama ya
Dola 600 milioni (Sh1.3 trilioni) kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya
Umma.
Wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mkataba
wa kibiashara na kampuni hiyo bila zabuni shindanishi kinyume cha sheria
hiyo ya manunuzi ya umma.
Hata hivyo, wakati wa usikilizwaji wa
kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwaita mahakamani jumla ya mashahidi
watano kujenga kesi yao, akiwamo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa
mamlaka hiyo, Kokutulage Kazaura.
Kwa upande mwingine, Mahakama
hiyo imeshindwa kutoa uamuzi wa uhalali wa shtaka la kutakatisha fedha
linalomkabili aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya na wenzake
wawili.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mshindi wa
Mashindano ya Urembo (Miss Tanzania), mwaka 1996, Shose Sinare na Sioi
Solomon ambao walikuwa wafanyakazi waandamizi wa Benki ya Stanbic tawi
la Tanzania.
Washtakiwa hao watatu wanadaiwa kutakatisha fedha
dola 6 milioni (1.2 bilioni) wakati Serikali ilipokopa Dola 550 milioni
(takriban Sh1.2 trilioni) kati ya mwaka 2012 na 2013 kutoka katika Benki
ya Standard ya Uingereza ambayo ni kampuni mama ya Stanbic.
Washtakiwa
hao kupitia kwa mawakili wao walihoji uhalali wa shtaka hilo na kuiomba
mahakama ilifute pamoja na mambo mengine wakidai kuwa halijakidhi
vigezo vya kisheria kuitwa shtaka la utakatishaji fedha.
Maombi
yao hayo yalitarajiwa kutolewa uamuzi jana na Hakimu Mkazi Emilius
Mchauru, anayesikiliza kesi hiyo, lakini uamuzi huo ulikwama na badala
yake ulipigwa kalenda hadi Aprili 27, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment