Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mtafungwa
Vijana 11 waliokuwa na shauku ya kujiunga na Chuo cha Polisi Moshi (MPA) wamejikuta wakitapeliwa kati ya Sh. milioni moja hadi milioni 1.5 kila mmoja, baada ya kulaghaiwa na mmoja wa askari mgambo mjini humo kuwa atawapatia nafasi ya kujiunga na chuo hicho.
Habari
za uhakika zilizopatikana mjini hapa jana na baadae kuthibitishwa na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mtafungwa na Mkuu wa
chuo hicho, Kamishna Mwandamizi Matanga Mbushi, zinaeleza kwamba, vijana
waliotapeliwa wanatokea mkoa wa Mbeya.
Kamanda Mutafungwa alisema jana
kwamba, Jeshi la Polisi halijatangaza nafasi za mafunzo hayo na kwamba
mtuhumiwa aliyefanya utapeli huo ambaye ni askari mgambo mkazi wa Mbeya,
amekamatwa mjini Moshi na anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kabla ya
kufikishwa mahakamani.
“Tunamshikilia
mgambo huyo katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi kwa ajili ya
kukamilisha taratibu za kumuhoji na tutamsafirisha jijini Mbeya kwenda
kujibu mahakamani tuhuma zinazomkabili. Hawa vijana walipohojiwa
walisema walichukuliwa eneo la Mbalizi, Mbeya,” alisema.
Kufuatia
tukio hilo, polisi mkoani Kilimanjaro wamelazimika kutafuta mawasiliano
ya wazazi wa vijana hao kwa ajili ya kutuma fedha za nauli za
kuwasafirisha kurudi nyumbani hadi hapo kesi ya msingi itakapofunguliwa
jijini Mbeya.
Wakati
vijana hao wanakamatwa katika chuo hicho, walikuwa wamefungashiwa vifaa
vyote muhimu kwa ajili ya kujiunga na Jeshi la Polisi.
Alipotafutwa
Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi, Mbushi ili kuzungumzia suala hilo,
alisema katika uchunguzi wao wa awali wamebaini kwamba kuna askari mmoja
mwenye cheo cha koplo kutoka mkoa wa Mbeya alihusika na alichukua fedha
hizo lakini hakuja Kilimanjaro.
Alisema
mgambo huyo alikamatwa baada ya kufika chuoni hapo akiwa ameambata na
vijana hao 11, wavulana wanane na wasichana watatu.
Aliwataka
wazazi kuelewa kwamba, nafasi za mafunzo ya polisi hazinunuliwi na wala
haziuzwi mitaani, bali muda unapofika huwa zinatangazwa na kuwataka
zinapotangazwa nafasi hizo waende wakaulize kwenye ofisi za wakuu wa
polisi wa mikoa na wilaya ili waweze kupata uhakika na kujulishwa hatua
wanazotakiwa kuzifuata ili kukidhi vigezo vya kujiunga na Jeshi la
Polisi.
Hili
ni tukio la pili la vijana kutapeliwa fedha wakilaghaiwa kutafutiwa
nafasi za kujiunga na mafunzo ya polisi, la kwanza likiwa ni 2015 vijana
90 kutoka jijini Dar es Salaam walipotapeliwa kwa njia hiyo.
0 comments:
Post a Comment