Rais John Magufuli juzi aliwazungumzia makada walioihama CCM wakati wa
mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopita, alipoeleza kuwa kuondoka kwao
pengine kulimsaidia kupata ushindi.
Bila kutaja majina ya
waliokihama chama, Magufuli alisema ni vyema wana CCM wakasahau tofauti
zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo na kuganga yajayo.
Rais
alisema hayo kwenye mkutano na viongozi wa CCM wa mikoa na wilaya zote
nchini, uliofanyika juzi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Alisema
kuna mengi yalitokea wakati wa uchaguzi huo na yalikidhoofisha chama na
hivyo kuna haja ya kuyasahau yaliyopita na kuangalia mbele katika
kukijenga chama.
“Lakini inawezekana wale walioamua kwenda kule walisaidia mimi kushinda,” alisema bila ya kufafanua.
Baadhi
ya wana CCM waliokihama chama hicho wakati wa uchaguzi huo ambao
ulikuwa na ushindani mkubwa kuanzia ndani ya chama hicho ni pamoja na
mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowasa aliyehamia Chadema, Frederick
Sumaye, ambaye kwanza alitangaza kujiunga na upinzani bila ya kutaja
chama na mapema mwaka huu kukabidhiwa kadi ya Chadema.
Mwingine
ni aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, Balozi Juma
Mwapachu, mawaziri, wabunge na madiwani, wengi wakijiunga na Chadema,
ambayo ilimsimamisha Lowassa kuwa mgombea wake wa urais akiungwa mkono
na vyama vya NLD, NCCR-Mageuzi na CUF vilivyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
Lowassa alionekana kuwa kinara kwenye harakati
za urais ndani ya CCM, akichuana vikali na Bernard Membe, lakini jina
lake halikufikishwa kwenye Kamati Kuu, ambayo ilitangaza majina matano,
akiwamo Magufuli, yaliyopelekwa Halmashauri Kuu ya chama hicho.
Kitendo
hicho kilifanya wajumbe wa Halmashauri Kuu kumpinga waziwazi mwenyekiti
wa CCM, Jakaya Kikwete na baada ya juhudi za wazee wa chama hicho, hali
ilitulia na Magufuli akaongoza kwa kura nyingi. Baadaye Lowassa
alitangaza kuhamia Chadema na kufuatiwa na wanachama kadhaa.
Alipotangazwa
mshindi wa Uchaguzi Mkuu, Magufuli alisema wakati akihutubia wanaCCM
kwenye ofisi ndogo ya chama hicho Lumumba jijini, alisema uchaguzi huo
ulikumbwa na hujuma zilizofanywa na wanafiki waliojificha ndani ya chama
hicho.
Alisema ni vema wanafiki hao wakajisalimisha kwa kutubu
kwa kuwa wamekigharimu chama hicho na kusababisha kiwe kwenye wakati
mgumu.
Dk Magufuli alisema anaona ni bora kuishi na mchawi
kuliko mnafiki, na kumuomba Kikwete asiwahurumie wanaokihujumu chama.
CCM walikidhoofisha chama
Juzi, akizungumza kwenye mkutano huo na
viongozi wa CCM ambao katika hali isiyokuwa ya kawaida hawakuvaa sare
zao za chama, Magufuli alisema waliokidhoofisha chama ni wana CCM
wenyewe na ndiyo maana wapinzani walitumia udhaifu huo kukisaliti.
“Tulithamini
fedha kuliko chochote. Wala hatukuuliza hizi fedha zimetoka wapi.
Tuliowapa miradi, walituchezea, tumejikaanga CCM kwa mafuta yetu
wenyewe. Kama tulifanya makosa, tusifanye tena,” alisema.
Aliwataka viongozi hao wa CCM kuanza kuzungukia maeneo yao ili kuwashukuru wananchi kwa ushindi na kukiimarisha chama.
“Kwa
kifupi, nyinyi ndiyo Serikali. Kiongozi yeyote mnayemuona hatekelezi
ilani yake, huyo hafai kwenye safari hii. Mimi niwaahidi hatutasita
kuchukua hatua kwa wale mtakaoona hawafai,” alisema.
Awali
Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana alisema Kamati Kuu ya CCM
imepokea ripoti ya uchaguzi huo wa Oktoba 25 kutoka mikoa yote na wiki
ijayo itafanyika tathmini ya maandalizi, mchakato wa kuwapata wagombea,
matokeo, upigaji kura na utangazaji wa matokeo.
Azungumzia Watumishi Hewa CCM
Kadhalika, Magufuli alimtaka Kinana kuanza kuchukua hatua za kuondoa wafanyakazi hewa ndani ya chama hicho.
“Na
mimi nina uhakika katibu mkuu hata kwenye chama wapo wafanyakazi hewa
kwa sababu watu ni wale wale, ni Watanzania wale wale. Kwa hiyo na wewe
uanze kuchukua hatua dhidi ya wafanyakazi hewa walioko kwenye chama,”
alisema.
Alisema Serikali inatumia zaidi ya Sh583 bilioni kulipa
mishahara, lakini mpaka sasa kuna wafanyakazi 7,700 hewa wakati
uchambuzi bado ukiendelea.
0 comments:
Post a Comment