Wabunge wa CCM jana waliibuka kidedea walipowazidi wenzao wa upinzani kwa kura za sauti “Siyooooo” kuikataa hoja ya kutaka matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja ‘live’ na televisheni.
Hiyo ilitokea jana wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha
bajeti ya Ofisi ya Rais (Tamisemi na Utumishi na Utawala Bora) na kuzua
mvutano mkali uliosababisha bajeti hiyo ipitishwe kwa utaratibu wa
wabunge kutohoji kitu chochote (guillotine).
Wakati hoja yao hiyo ikipingwa kila kona, tangu kuanza kwa Bunge la
Bajeti, wabunge hao wa upinzani sasa wamebuni mbinu mpya ya kujirekodi
wenyewe wakati wakichangia mijadala mbalimbali bungeni na kurusha sauti
zao kwenye mitandao ya kijamii na kupeleka sauti hizo kwenye redio
zilizopo katika maeneo ya majimbo yao.
Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Salehe ndiye aliyeibua hoja hiyo
akitaka kushika mshahara wa waziri kwa maelezo kuwa kuzuia Bunge
kurushwa ‘live’ ni kinyume na utawala bora na haki ya kupata habari.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema),
Mchungaji Peter Msigwa, Masoud Abdalla Salim (Mtambale-CUF), Rose Kamili
(Viti Maalumu -Chadema), Ester Matiko (Tarime Mjini – Chadema) na Mussa
Mbarouk (Tanga Mjini – CUF).
Wabunge wa CCM waliopewa nafasi na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew
Chenge kuchangia hoja hiyo ni Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini), Kangi
Lugola (Mwibara), Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) pamoja na Waziri Ofisi
ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki.
Ilivyokuwa Bungeni
Baada ya Salehe kutaka ufafanuzi wa kina huku akisisitiza kuwa
uamuzi huo unakiuka Katiba ya nchi na haki ya kupata habari, Kairuki
alisema kwa mujibu wa Ibara ya 18 na 100 ya Katiba zinazozungumzia uhuru
wa kupata habari, uamuzi huo ni sahihi na hakuna mwananchi aliyenyimwa
taarifa.
Maelezo hayo yalipingwa na Salehe, safari hii akifafanua kuwa
matangazo ya Bunge yanarekodiwa kwa saa saba na kurushwa na Televisheni
ya Taifa (TBC) kwa saa moja tu, huku wabunge wa upinzani wakiondolewa na
kuonyeshwa wa CCM pekee.
Alitaka vyombo vya habari vya elektroniki kuruhusiwa kurekodi
shughuli za Bunge na kurusha maudhui wanayoyataka, badala ya kupewa
video na studio ya Bunge ambayo huondoa michango na hoja za wapinzani.
Mchungaji Msigwa, Masoud Abdallah, Kamili, Matiko waliungana na
Salehe na kusisitiza kuwa nchi nyingi barani Afrika zinarusha ‘live’
matangazo ya Bunge huku wakihoji sababu za TBC kurusha moja kwa moja
harusi na kushindwa kuonyesha shughuli za Bunge.
Mbarouk alikwenda mbali akitaka Bunge kuanza shughuli zake usiku
ili kuendana na utetezi wa Waziri wa Habari, Nape Nnauye kuwa usiku
wananchi wengi wanakuwa majumbani mwao hivyo wanapata nafasi nzuri ya
kufuatilia Bunge.
Matiko: Juzi Rais John Magufuli kazindua Daraja la
Kigamboni, TBC ilikata matangazo ya Bunge ili kuonyesha uzinduzi huo.
Yaani ya kwenu mnataka yaonyeshwe ila haya ya Bunge yasionekane.
Mnakiuka demokrasia.
Ghasia: Demokrasia siyo Bunge kuonyeshwa ‘live’. Wakulima na wafugaji hawawezi kuona Bunge asubuhi ndiyo maana yanarushwa usiku.
Serukamba: Mbona wabunge wa Chadema wanaonyeshwa katika
matangazo ya TBC. Hoja kwamba maagizo ya Serikali hayatawafikia
watendaji si kweli.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju alisema wapinzani
hawajiamini na hawaaminiki huku akiwataka wasome ibara ya 100 ya Katiba;
“Bunge kuonyeshwa au kutoonyeshwa hakuongezi kitu jimboni. Wanaozungumza ni wabunge siyo televisheni.”
Akihitimisha hoja, Kairuki alipinga maelezo ya Salehe na kutoa mfano wa nchi ambazo matangazo ya Bunge hayarushwi moja kwa moja.
Kutokana na mvutano huo Chenge aliwahoji wabunge wanaoafiki hoja ya
Salehe waseme “ndiyooo”, wapinzani pekee wakasema ndiyoo, aliposema
wasioafiki waseme siyo, wabunge wa CCM kutokana na wingi waliitikia kwa
sauti kubwa siyoooo, na Chenge akasema anadhani wasioafiki wameshinda.
Wapinzani Waamua Kujirekodi kwa simu
Kwa zaidi ya mara tano,wabunge wa upinzani wameshuhudiwa
wakijirekodi ndani ya ukumbi wa Bunge kwa kutumia simu zao za mkononi,
wanapotoka nje huulizana kama wameshatumia video na sauti hizo katika
mitandao ya kijamii.
Juzi, Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara baada ya kumaliza
kuchangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais (Tamisemi na Utawala Bora)
alirusha sauti yake katika mitandao ya kijamii na kusema hiyo ni moja ya
njia ya kuwafanya wananchi wajue kinachoendelea bungeni
0 comments:
Post a Comment