Waumini
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, wamesali Jumapili ya tatu bila kuwapo kwa
Askofu wao, Josephat Gwajima,lakini wameshtushwa na taarifa kuwa
kiongozi huyo wa kiroho ni mgonjwa na anapata matibabu nje ya nchi.
Waumini
hao walisema wamekuwa wakisikia kuwa askofu wao anatafutwa na Jeshi la
Polisi na juzi wamesikia kuwa anapata matibabu nje ya nchi wakati wao
hawajatangaziwa rasmi kuhusu taarifa hizo.
Juzi,
Wakili wa Askofu Gwajima, Peter Kibatala aliileza Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu kuwa mteja wake hakufika mahakamani kwa kuwa yuko nje ya
nchi kwa ajili ya matibabu.
Askofu
Gwajima alitakiwa kufika mahakamani hapo anakokabiliwa na kesi ya
kumtolea lugha chafu Askofu Mkuu Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi,
Cyprian Mkeha.
Mbali
na taarifa za kuumwa, pia Gwajima anatafutwa na Polisi baada ya
kusambaa kwa sauti inayosikika kama yake ikitaka Rais Mstaafu, Jakaya
Kikwete afikishwe mahakamani kwa yote yaliyofanyika katika utawala
wake.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa atalizungumzia suala hilo leo Jumatatu.
Katika
ibada ya jana, kama kawaida, Mchungaji Adriano Edward hakuwaeleza
chochote waumini wa kanisa hilo kuhusu alipo Askofu Gwajima wala hali ya
afya yake.
Mchungaji
Adriano alipotakiwa kuzungumzia suala la afya ya Gwajima, alisema
kupitia msaidizi wake kuwa hawezi kuzungumza chochote na vyombo vya
habari.
0 comments:
Post a Comment