Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesitisha utoaji wa vibali vya uvunaji
wa mbao kutoka katika mashamba nane ya miti ya kupandwa yanayosimamiwa
na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Serikali kupitia
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) chini ya Wizara ya Maliasili
na Utalii inamiliki mashamba ya miti ya kupandwa 18, na kati ya hayo
uvunaji umekuwa ukifanyika katika mashamba nane ambayo ni
- Sao Hill (Mufindi),
- Buhindi (Sengerema),
- Meru/Usa (Arumeru),
- West Kilimanjaro (Hai),
- Shume (Lushoto),
- North Kilimanjaro (Rombo),
- Kiwira (Rungwe) na
- Kawetire (Mbeya Vijijini).
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Julai 8, 2016) na
kufafanua kwamba usitishaji huo unalenga kutathmini taratibu, kanuni na
vigezo sahihi vinavyotakiwa kutumika katika kugawa malighafi kutoka
kwenye mashamba hayo.
Amesema wadau wote wa viwanda vinavyojikita
katika malighafi ya misitu na hususan wamiliki wa viwanda vya kupasua
mbao wanashauriwa kuwa watulivu wakati utaratibu huu ukifanyiwa mapitio
na umma utatangaziwa rasmi pindi uboreshaji huo utakapokamilika.
0 comments:
Post a Comment