PAMOJA na majigambo na lugha za kejeli, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
amesalimu amri mbele ya Bunge na hatimaye chombo hicho kumsamehe baada
ya kuomba radhi na kuonyesha unyenyekevu, alipoitwa kuhojiwa.
Mbali na kiongozi huyo, bunge pia limewasamehe Kiongozi wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mkuu wa Wilaya Arumeru, Alexander
Mnyeti, baada ya kufuata nyayo za Makonda kwa kukiri kutekeleza na
kuomba radhi kwa kutoa lugha isiyofaa.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Almas
Maige akiwasilisha bungeni mjini hapa jana taarifa kuhusu mashauri
yanayowahusu watatu hao, alipendekeza Bunge liwasamehe kutokana na
uungwana wao wa kukiri, kuomba radhi na kujutia makosa yao walipofika
mbele ya kamati hiyo kwa ajili ya kuhojiwa.
Akizungumzia shauri la kigogo huyo, aliyekuwa anatuhumiwa kusema wabunge
wanasinzia bungeni, Maige alisema kamati yake ilikuwa na hadidu mbili
za rejea, kama ni kweli alitamka maneno hayo yaliyolalamikiwa na wabunge
na hatua za kisheria zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya yake kama
alitenda kosa hilo.
Alisema chanzo cha malalamiko dhidi yake ni hatua aliyoichukua ya kutaja majina ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya.
Alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari ofisini kwake jijini
Dar es Salaam, kiongozi huyo wa serikali aliulizwa hatua anazozichukua
dhidi ya baadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya
na wengine walikuwa wameanza kutajana wao wenyewe bungeni.
Kwa mujibu wa Maige, katika kujibu swali hilo, alisema: "... zingine ni
mbwembwe tu, unajua mle ndani (bungeni) wakati mwingine wanachoka na
kusinzia lazima kuwe na watu kidogo akili zao zinawasaidia kuamka,
kucheka na kufurahi maisha yanaendelea."
Maige alisema kiongozi huyo alifika mbele ya kamati yake Machi 29, mwaka
huu, majira ya saa nne asubuhi kwenye Ukumbi wa Spika na kusomewa
tuhuma dhidi yake na kukiri kwamba ni kweli alitoa kauli hiyo.
Alisema katika maelezo yake alionyesha kujutia kauli hiyo ambayo
iliwakwaza na kuwavunjia heshima wabunge, hivyo aliomba radhi na kueleza
kuwa hata kabla ya kuitwa mbele ya kamati, tayari alikuwa ameandika
barua kwa Spika ya kuliomba radhi Bunge.
Maige alinukuu sehemu ya maelezo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuomba
radhi kuwa ni: "... najisikia vibaya kusimama mbele yenu kwa kuwakwaza
na kuwavunjia heshima ambayo sikupaswa kufanya hasa kwa watu ambao
mmekuwa walezi na ni watu ambao mnanitegemea nifanye vizuri kwa ajili ya
kuwawakilisha vijana wengine.
"Itakumbukwa baada ya kauli yangu, nilichukua jukumu la kuandika barua
kwa Mheshimiwa Spika, baada ya kusikiliza mjadala katika Bunge na
kumwomba radhi kwa kitendo cha kauli yangu niliyoitoa wakati nikijibu
swali pale ambapo mwandishi alitaka kujua mambo kadhaa yaliyofanyika.
"Kwa hiyo, akili yangu ilikuwa na mtazamo wa namna hiyo, haikuwa na
mtazamo wa kulidharau Bunge, haikuwa na mtazamo wa kumvunjia heshima
mbunge yeyote yule na kwa kweli najisikia vibaya sana kusimama mbele
yenu na ninaomba radhi sana sana kwa kauli niliyoitoa na tafsiri
iliyopatikana."
Kutokana na maelezo hayo, Maige alisema kamati yake imejiridhisha bila
shaka yoyote kwamba maneno ya Mkuu wa Mkoa huyo yalivunja haki na
kudharau mamlaka ya Bunge.
Alisema kitendo cha kutamka maneno hayo ni cha kudharau, kudhalilisha na kulifedhehesha Bunge.
Hata hivyo, licha ya kukiuka masharti ya kifungu cha 26(e) cha Sheria ya
Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge (Sura ya 296), Maige alisema Bunge
limeazimia Mkuu wa Mkoa huyo asamehewe kutokana na kitendo chake cha
kiungwana cha kukiri na kujutia kosa lake na kuliomba radhi Bunge mbele
ya kamati yake.
Alisema kamati yake imezingatia ukweli kwamba Mkuu wa Mkoa huyo
hakuisumbua kwa namna yoyote ile bali alikuwa mtii na alitoa ushirikiano
mkubwa kwa kamati.
Alisema kamati pia imezingatia kuwa kiongozi huyo wa serikali hakuwa na
dhamira ya kulidharau wala kulidhalilisha Bunge kama ambavyo
ilichukuliwa.
Mbunge huyo wa Newala (CCM) alisema kamati imezingatia kuwa Mkuu wa Mkoa
huyo alikuwa hajawahi kutenda kosa kama hilo na kufikishwa mbele ya
kamati na pia amekiri kosa lake na kuomba radhi.
Alisema msamaha wake pia umezingatia kitendo cha Mkuu wa Mkoa huyo
kuandika barua kwa Spika kuomba radhi, uzoefu wa mabunge mengine ya
Jumuiya ya Madola kuhusu adhabu kwa mtu ambaye amekiri kosa la kudharau
Bunge na kuomba msamaha.
SHAURI DC MNYETI
Akizungumzia shauri la DC Mnyeti, Maige alisema chanzo cha malalamiko
hayo ni taarifa ya Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa
iliyowasilishwa Februari 3, mwaka huu na kuanisha changamoto za
mapendekezo ya kuzitatua ikiwa ni pamoja na suala la Wakuu wa Mikoa na
Wilaya kutumia vibaya mamlaka yao.
Maige alisema kuwa katika taarifa hiyo, kamati ilipendekeza waziri
mwenye dhamana awapatie semina viongozi hao wa serikali namna ya
kutekeleza majukumu yao.
Kutokana na masuala mbalimbali yaliyojadiliwa bungeni kuhusiana na jambo
hilo, Maige alisema ndipo Mnyeti alipoandika katika ukurasa wake wa
mtandao wa Facebook akiyaita mapendekezo hayo ni ya upuuzi mtupu na
kwama wabunge hawajielewi na anawashauri wafanye kazi zao.
Akinukuu maneno hayo, Maige alisema: "Upuuzi mtupu. Wabunge hawa
hawajielewi. Nawashauri fanyeni kazi zenu za wengine waachie wenyewe."
Alisema kuwa Mnyeti aliitwa mbele ya kamati hiyo Aprili 6, mwaka huu na
kuhojiwa kuhusu tuhuma zilizomkabili na alikiri kuandika maneno hayo na
kumiliki akaunti ya Facebook iliyoandika maneno yaliyolalamikiwa.
Alisema kuwa baada ya maelezo, shahidi aliomba radhi kwa Bunge na kusema hana ubavu wa kushindana nalo.
Maige alinukuu maneno ya Mnyeti akisema: "...Mheshimiwa Mwenyekiti, basi
naomba sasa kamati yako itumie busara na ninaomba radhi kwamba limekuwa
kubwa lakini halikuwa kusudio langu tangu awali kwamba sasa nilikwaze
Bunge kwa 'style' (mtindo) hiyo.
"Mimi naomba radhi kamati yako, itumie busara zake lakini lengo kutoka
moyoni kwangu halikuwa katika hali hiyo ambayo limechukuliwa... Nikiri
kuwa ni madhaifu yangu sikutenda kiungwana, naomba kamati inisamehe
kuanzia sasa na kuendelea haitajirudia tena. Kwa hiyo, binafsi niiombe
kamati yako kwa nafasi ya kipekee ione umuhimu wa kunisamehe..."
Kutokana na maelezo hayo ya Mnyeti, Mkuchika alisema kamati yake
imethibitisha kuwa Mkuu wa Wilaya huyo aliingilia uhuru na kuvunja haki
za Bunge kinyume cha kifungu cha 26(e) cha Sheria ya Kinga, Haki na
Madaraka ya Bunge.
Alisema kitendo cha kuandika maneno hayo ni cha dharau, kudhalilisha na
kulifedhehesha Bunge lakini kwa kuzingatia kwamba Mnyeti hakuisumbua
kamati na alikuwa mtii na kutoa ushirikiano na hajawahi kutenda kosa
jingine la aina hiyo, Bunge limeazimia kumsamehe.
Februari 8, mwaka huu, Bunge lilipitisha maazimio ya kuwaita bungeni na
kuwahoji Makonda na Mnyeti kutokana na hoja ya Mbunge wa Ukonga, Mwita
Waitara (Chadema) aliyewatuhumu viongozi hao wa serikali kuudharau
mhimili huo na ikithibitika, wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria
zilizopo.
SHAURI LA MBOWE
Akizungumzia shauri la Mbowe, Mkuchika alisema lilianzia Aprili 4, mwaka
huu wakati wa mkutano wa kwanza wa Bunge la Bajeti ambao ulikuwa na
uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ambapo baadhi ya
wabunge walionekana kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu.
Alisema Mbowe alinukuliwa na vyombo vya habari akitoa maneno ya utovu wa
nidhamu kwa kudharau Mamlaka ya Spika na kutoa maneno ya kuudhi dhidi
ya wabunge wengine, kitendo ambacho alikifanya akiwa nje ya ukumbi wa
Bunge baada ya uchaguzi huo.
Katika uchunguzi wa kamati yake, Mkuchika alisema walijiridhisha kuwa
Mbowe alitamka maneno: "... Spika amevunja Kanuni za Bunge, sheria
hazikuheshimiwa, ubabe umetumika... ni mkakati wa kiserikali, tunajua
Rais anahusika, Waziri Mkuu anahusika, viongozi wa chama chao
wanahusika...
"...tumeleta wagombea wazuri sana wawili 'very competent', wamepigiwa
kura za hapana kwa sababu ulikuwa mkakati wa Chama Cha Mapinduzi,
tumeona ujinga na upumbavu mtupu... uchaguzi huu umekuwa wa kijinga"
Mkuchika alisema kuwa baada ya kumuita mbele ya kamati, Mbowe alikiri wazi kuwa alitamka maneno hayo na akaliomba radhi Bunge.
Licha ya kumtia hatiani kiongozi huyo wa upinzani kwa kudharau mamlaka
ya Spika, Mkuchika alisema Bunge limeazimia kumsamehe kutokana na
kitendo chake cha kuonyesha ushirikiano na kuomba radhi huku
likimkumbusha kuwa anatakiwa kuwa mfano kwa wengine anaowaongoza.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) na Mbunge wa Hai, alitakiwa na Spika kufika mbele ya kamati
hiyo mwanzoni mwa mwezi uliopita baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi
Lugola (CCM) kulamika bungeni kuhusu kauli zake hizo zilizomtia hatiani.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza HapaFollow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment