Thursday, 7 April 2016

#YALIYOJIRI>>>Serikali Yasema Itawafukuza Kazi Maofisa wa Serikali Wanaowawekea Vikwazo Waandishi wa Habari.Fahamu zaidi hapa.

Serikali  imesema itawafukuza kazi maofisa wa Serikali ambao wanaweka vikwazo na kuwakwamisha waandishi wa habari kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kupata habari na taarifa mbalimbali kutoka serikalini.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliyasema hayo jijini Mwanza wakati alipozungumza na wadau wa utamaduni, habari na michezo kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza.

Alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi wa swali lililoulizwa na Mwandishi wa Habari wa ITV/ Radio One anayefanyia kazi zake mikoa ya Kanda ya Ziwa, Cosmas Makongo ambaye alitaka apate msimamo wa Serikali juu ya hatua zitakazochukuliwa na serikali kutokana na wimbi la unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali kwa waandishi wa habari nchini.

Makongo alisema akiwa wilayani Chato mkoani Geita hivi karibuni alizuiliwa kuandika habari na ofisa mmoja wa Serikali hadi pale atakapopata kibali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya.

“Kumeibuka wimbi la unyanyasaji wa kijinsia kwa waandishi wa habari, ukifika Chato huandiki habari mpaka upate kibali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya, nilizuiliwa kuandika habari hivi karibuni wakati nafanya habari ya uchunguzi wa mabilioni ya fedha wilayani humo,” alisema Makongo na kuhoji,

 “Mheshimiwa Waziri tukiendelea kusubiri vibali kutoka kwa watawala je, tutafichua maovu?” 

Nape alisema kuwa msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ni kuvitumia vyombo vya habari katika kufichua maovu yanayofanywa na baadhi ya watu katika jamii. 

“Kama kuna Ofisa wa Serikali anaweka kizuizi kwa mwandishi wa habari ili asipate habari na kushindwa kutimiza wajibu wake tutamfukuza kazi,” alisema Nape.

Aliwataka maofisa wa habari kote nchini wawe tayari kutoa taarifa mbalimbali za maendeleo zilizopo kwenye maeneo yao kwa wakati ili waandishi wauhabarishe umma.

0 comments:

Post a Comment