Friday, 1 April 2016

#YALIYOJIRI>>>Taarifa Rasmi Ya TAKUKURU Kuhusu Kumfikisha Mahakamani Mbunge wa Sumve, Richard Mganga Ndassa Kwa Tuhuma za Rushwa.Fahamu zaidi hapa.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) leo tarehe 1/4/2016 imemfikisha Mahakamani Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa Mbunge wa Sumve ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Mtaji na Uwekezaji kwa kosa la kushawishi na kuomba Rushwa ya Shilingi Milioni thelathini (30,000,000/-) kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15 (i)(a) na (2).

Akiwa kama mjumbe wa Kamati ya Mtaji na Uwekezaji tarehe 13/3/2016 Mhe. Ndassa alimwomba rushwa ya shilingi Milioni 30 kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Felchesmi J. Mramba ili amsaidie kuwashawishi wajumbe wengine wa Kamati ya Mtaji na Uwekezaji kupitisha bila kipingamizi taarifa ya TANESCO kwa mwaka 2015/2016.

Mbunge huyo amefunguliwa kesi namba 118/2016 na alisomewa mashtaka hayo na Wakili wa TAKUKURU Dennis Lekayo akishirikiana na Emmanuel Jacob katika Mahakama ya Kisutu mbele ya Mhe. Hakimu Emirius Mchauro.

Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kupata mdhamini mmoja na kulipa shilingi milioni 10. Uchunguzi wa shauri hili bado unaendelea na kesi hii itatajwa tena tarehe 18/4/2016.
 
IMETOLEWA NA
OFISI YA AFISA UHUSIANO
TAASISI YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA, MAKAO MAKUU
1 APRIL, 2016.

0 comments:

Post a Comment