Wednesday, 9 November 2016

#MICHEZO>>>SIMBA yakiri kuzidiwa nguvu na PRISONS ya Mbeya.Fahamu zaidi hapa.

Klabu wa Simba kupitia kwa nahodha wa timu Jonas Mkude imekiri kuzidiwa uwezo na mbinu za kisoka na Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliopigwa leo Jijini Mbeya na kushuhudia Simba ikilala kwa kipigo cha mabao 2-1.

Nahodha wa Simba, Jonas Mkude

Akizungumza baada ya mchezo huo, Mkude amesema kuwa lengo la timu yake ilikuwa ni ushindi, na kiujumla timu ilikuwa na maandalizi yote lakini imefungwa kimchezo, kwa kuwa licha ya wao kuonesha kandanda safi kipindi cha kwanza, Prisons waliwazidia nguvu kipindi cha pili na kuweza kupata mabao mawili.

Katika mchezo huo Simba ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Jamal Mnyate dakika ya 43 kwa kichwa akimalizia kros ya Shiza Kichuya.

Prisons walisawazisha katika dakika ya 47 na kupata bao la ushindi dakika ya 64 kupitia kwa Victor Hangaya aliyefunga mabao yote mawili kwa kichwa akimalizia kros zilizoshindwa kuokolewa na mabeki wa Simba.

Kwa upande wake kocha msaidizi wa Simba Jackson Mayanja amesema licha ya kufungwa, anashukuru kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa inaongoza ligi na kwamba anasikitishwa kwa kumaliza vibaya licha ya kuanza vizuri huku akisema kuwa bado ana matumaini kwa kuwa bado kuna mzunguko wa pili.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kupoteza mchezo wa pili mfululizo na hivyo kubaki na pointi zake 35 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 30 ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa kesho Alhamis katika dimba la Uhuru Dar es Salaam.

Katika mchezo mwingine uliopigwa leo, Azam imeishushia Mwadui kipigo cha mabao 4-1 katika dimba la Mwadui Complex na kuifanya ifikishe pointi 25 katika nafasi ya tatu.

0 comments:

Post a Comment