Maofisa wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Juma Matandika na Martine Chache, leo Jumatano wamepandishwa
kwenye Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam wakituhumiwa kuomba rushwa ya
shilingi milioni 25 kwa timu ya soka ya Geita Gold ili kuisaidia kupanda
daraja.
Wahusika hao walifikishwa mahakamani
hapo mapema na baadaye walipandishwa kizimbani kwa tuhuma hizo ambapo inadaiwa
walitenda kosa hilo Februari 4, mwaka huu kwenye ofisi za TFF zilizopo Karume
jijini Dar.
Juma Matandika
Kesi hiyo ambayo ilisomwa mbele ya
Hakimu Mkazi Huruma Shahidi ilisimamiwa na wakili Leonard Swai akiwakilisha
upande wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wakati upande wa
serikali iliwakilishwa na wakili Odesa Horombe. Upande wa watuhumiwa walitetewa
na wakili Claudia Nestory.
Katika tuhuma hizo, watuhumiwa
wanadaiwa kutenda kosa hilo kwa kuomba rushwa kwa viongozi wa Geita Gold, Salum
Kulunge na Costantine Molandi kwa ajili ya kushinikiza TFF wawapandishe Ligi
Kuu Bara kutoka Ligi Daraja la Kwanza katika ligi ya msimu uliopita.
Mara baada ya kusomewa mashtaka hayo,
watuhumiwa wote walikana kutenda kosa hilo ambapo kesi imeahirishwa hadi
Novemba 30, mwaka huu, watuhumiwa wote wameachiwa kwa dhamana ya shilingi
milioni 5 kila mmoja.
0 comments:
Post a Comment