Thursday 12 May 2016

#MICHEZO>>>>AZAM NA SIMBA ZAPIGANA VIKUMBO KUMUWANIA KOCHA WA HARAMBEE STARS.Fahamu zaidi hapa.

Na Baraka Mbolembole
Azam FC na Simba SC zimeingia katika vita ya kumuwania mkufunzi, Bobby Williamson raia wa Scotland. Inaonekana wazi kuwa Azam itaachana kwa mara ya tatu ndani ya miaka minne na mkufunzi wake wa sasa Muingereza, Stewart Hall.

Williamson, 54, mchezaji wa zamani wa klabu za Clydebank, Rangers, West Brom, Rotherham United na Kilmarnock anatafutwa pia na Simba ili achukue nafasi iliyoachwa na Dylan Kerr. Mganda, Jackson Mayanja amekuwa akikaimu nafasi ya kocha tangu mwezi Januari yeye ataendelea kubaki katika timu hiyo kama kocha msaidizi.

Habari za ndani ambazo nimezipata kutoka kwa chanzo chetu cha karibu katika timu hiyo zinadai kwamba, Azam wanajaribu kumshawishi Williamson kuachana na kazi ya kuinoa Kenya na kuja kuisaidia timu hiyo katika ligi kuu na michuano ya CAF msimu ujao.

Williamson ambaye alicheza jumla ya michezo 402 na kufunga magoli 138 wakati wake wa uchezaji ni kocha aliyepata mafanikio makubwa zaidi katika michuano ya CECAFA Challenge Cup akiwa na timu ya Taifa ya Uganda ‘Cranes’ kati ya mwaka 2008 hadi 2013. Alishinda mataji manne ya CECAFA katika miaka yake mitano (2008, 2009, 2011 na 2012).

Baada ya Uganda kushindwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti na Zambia katika mchezo wa ‘play off’ kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2013, Williamson aliachana na timu hiyo huku Waganda wakimsifu kwa kazi yake nzuri katika kipindi cha miaka mitano aliyofanya kazi kama mkufunzi mkuu wa Cranes.

Kocha huyo wa zamani wa Kilmarnock, Hibernian, Plymouth Argyle na Chester City alijiunga na Gor Mahia FC ya Kenya mwaka 2013 na kuisaidia kuipa ubingwa wa Ligi kuu mwaka 2014.
August 2014, Shirikisho la soka nchini Kenya likamteua, Williamson kuwa meneja wa timu ya Taifa ‘ Harambee Stars’ majukumu ambayo anayo hadi sasa. Je, Simba na Azam ni timu gani itafanikiwa kumleta mtaalamu huyo wa ufundishaji katika VPL? Tusubiri na tuone.

0 comments:

Post a Comment