Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amefungua duka la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika
Hospitali ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambalo litakuwa na uwezo wa
kuhudumia hospitali 524 katika mikoa ya Lindi, Mtwara na wilaya ya
Tunduru mkoani Ruvuma.
Akizindua
duka hilo leo (Jumamosi, Julai 16, 2016) Waziri Mkuu amesema duka hilo
litaendelea kuboresha huduma za upatikanaji wa dawa kwa gharama nafuu
katika hospitali, vituo vya afya na zahanati katika wilaya ya Ruangwa
pamoja na mikoa na wilaya za jirani.
Duka
hilo ni la sita kufunguliwa tangu Mhe. Rais Dk. John Magufuli alipotoa
agizo kwa MSD kufungua duka la dawa ndani ya Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, ambapo mengine yako katika mikoa ya Mwanza (Sekou Toure),
Arusha (Mount Meru), Mbeya (karibu na hospitali ya mkoa) na Geita
(hospitali ya wilaya ya Chato).
“Duka
hili litasaidia kufikiwa kwa malengo ya Serikali ya kuboresha huduma za
afya kwa wananchi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba
kwa wakati na kwa gharama nafuu, hivyo nawaomba mlitumie duka hili,” amesema.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa benki ya NMB, kikosi cha
SUMA JKT na MSD kwa kufanikisha ujenzi wa duka hilo ambalo litaimarisha
upatikanaji wa dawa kwa uharaka.
Awali
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema kuanzishwa kwa duka
hilo kutaongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa gharama nafuu ,
hivyo kuondoa usumbufu kwa wagonjwa wa kwenda kuzitafuta katika ya
mbali na kwa bei kubwa.
“Nitoe
mfano wa tofauti wa bei za dawa kati ya maduka yetu na mengine, dawa ya
sindano ya diclofenac tunauza sh. 250 huku mitaani ni sh. 1,000 hadi
1,500 , ampliclox dozi moja MSD sh. 1,500 mtaani sh. 3,500 na
Ciprofloxacin MSD sh. 100 na mtaani sh. 500 hadi 1,000,” amesema.
Mkurugenzi
huyo amesema lengo la maduka hayo si kuuza dawa reja reja, nia yao ni
kuziuzia hospitali, vituo vya afya na Zahanati ili wagonjwa wanapokwenda
huko kupatiwa huduma wasikose dawa kwa wakati.
Akizungumzia
kuhusu gharama za ujenzi wa duka hilo Bwanakunu mesema umegharimu
sh.milioni 59 ambapo kati yake MSD imetoa sh. milioni 29 na benki ya NMB
imetoa sh. milioni 30.
“Mbali
na gharama za ujenzi MSD tumenunua na kufunga vifaa vya TEHAMA kwa sh
milioni 17 na mtaji wa dawa wa sh. milioni 37, ambapo imetenga sh.
milioni 100 kwa ajili ya dawa za duka hilo.
Amesema
duka hili litaendeshwa na kusimamiwa na MSD kwa muda wa mwaka mmoja na
kisha wataikabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa ajili ya
kuliendeleza ambapo litaisaidia katika kuiongezea mapato.
0 comments:
Post a Comment