Mke
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Janeth Magufuli
aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Sewahaji ya Hospitali ya Taifa
Muhimbili Jijini Dar es Salaam ameruhusiwa na kurejea nyumbani leo
tarehe 11 Novemba, 2016 baada ya afya yake kuimarika.
Kabla
ya kuondoka katika wodi ya Sewahaji alikokuwa amelazwa Mama Janeth
Magufuli amewashukuru Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa matibabu mazuri aliyoyapata na pia amewashukuru Watanzania
wote kwa kumuombea afya njema.
"Namshukuru
sana Mungu kwamba afya yangu imeimarika, pia napenda kuwashukuru
Madaktari na Wauguzi, nimepata huduma nzuri sana maana siku nilipoletwa
hapa nilikuwa sina fahamu na hali yangu ilikuwa mbaya lakini
mmenipigania na leo narudi nyumbani nikiwa na afya imara.
"Naomba
pia niwashukuru Watanzania wote kwa kuniombea, nawahakikishie kuwa sasa
nipo vizuri na madaktari wameniruhusu nirudi nyumbani ambako
nitamalizia matibabu yangu" amesema Mama Janeth Magufuli.
Mama Janeth Magufuli alilazwa hospitalini hapo tangu Juzi tarehe 09 Novemba, 2016 baada ya kuugua ghafla na kupoteza fahamu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Novemba, 2016
0 comments:
Post a Comment