Thursday, 3 November 2016

#YALIYOJIRI>>>>Ufisadi Wagubika Shirika la Posta.....Bodi Yabaini Mikataba Mibofu, Rushwa na Upendeleo katika Ajira.Fahamu zaidi hapa.

Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Posta Tanzania (TPC) imebaini madudu lukuki, ikiwamo mikataba mibovu, idadi kubwa ya wafanyakazi wenye elimu ya chini, rushwa na kuajiri kwa upendeleo. 
Akizungumza na wanahabari jana, mwenyekiti wa bodi hiyo, Dk Haruni Ramadhani alisema shirika linakabiliwa na “maradhi” mengi ambayo kama hayatashughulikiwa ipasavyo yanaweza kusababisha malengo kutotekelezwa kwa ufanisi. 
Kutokana na madudu hayo, bodi imeipa miezi sita menejimenti ya TPC kurekebisha kasoro hizo na kinyume na hapo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa. 
“Tumebaini Shirika la Posta lina uwezo na fursa kubwa kama tutaitumia vizuri kuchangia Pato la Taifa. Ni shirika ambalo limesambaza huduma zake toka ngazi ya Taifa, kata na vijiji. Posta ina mizizi mingi mikubwa na imara,” alisema. 
“Kinachokosekana ni utashi na kujituma, ubunifu na utendaji kazi kwa weledi na umakini. Lazima sasa tubadilike, tuache kufanya kazi kwa mazoea, uzembe, ubinafsi, ufisadi, wizi na rushwa. Vitu hivi lazima tuambizane ukweli bila kuoneana aibu. Havina nafasi tena Posta,” alisema. 
Mikataba Mibovu 
Dk Ramadhani alisema wakati bodi hiyo ikiendelea na uchunguzi, imebainika shirika hilo liliingia mikataba mibovu ukiwamo ule wa kati ya TPC na kampuni ya Wande Printing and Packaging. 

Katika mkataba huu, bodi ilibaini kuwa Wande Printing and Packaging walipangisha jengo la ghorofa tatu (mali ya shirika) kwa Sh1.8 milioni kwa mwezi, kwa muda wa miaka mitatu ambayo ni sawa na Sh64.8 milioni. 
Alisema baadaye, mwekezaji alifanya ukarabati wa jengo kwa Sh398 milioni, hivyo ili kufidia fedha hizo, mkataba huo ulieleza Wande Printing and Packaging itakaa kwenye jengo hilo bila kulipa kwa miaka 20 ili kufidia fedha zake. 
Mwenyekiti huyo alisema mkataba mwingine ni kati ya TPC na kampuni ya Universal G & G ambao ulihusisha upangishaji wa jengo lililopo kitalu namba 416 Block G, Ubungo. Alisema katika mkataba huo Universal G & G na TPC waliingia mkataba wa kudumu na TPC ina hisa asilimia 25 na Universal asilimia 75. 
Kaimu Posta Masta wa TPC, Fortunatus Kapinga alisema waliingia kimakosa mkataba wa jengo la Posta lililo karibu na Mawasiliano Tower, na sasa wapo kwenye utaratibu wa kuzungumza na mwanasheria wa kampuni.

Pamoja na mikataba mibovu, Dk Ramadhani alisema baadhi ya watumishi wa shirika hilo wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kufanya malipo hewa kwa wastaafu wa Shirika la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wakitumia mfumo wa Post Giro. 
Post Giro ni mfumo wa kizamani wa malipo kutoka benki moja kwenda benki nyingine na mlipaji ndiye huidhinisha malipo yote. 
Mwenyekiti huyo aliyataja madudu mengine waliyobaini ndani ya shirika hilo kuwa ni kuwepo na tabia ya kupeana ajira kwa upendeleo, kupandishwa vyeo kwa rushwa, fedha au rushwa ya ngono. 
“Kwa mfano vijana walioteuliwa na ofisi ya General Manager, Corperate Resource Management baadhi yao wana dalili za kujihusisha na rushwa. Mfano watumishi waliokuwa na vyeti feki wengi wao walisaidiwa kuviondoa katika majalada yao,” alisema.
Pamoja na madudu hayo mwenyekiti huyo alisema wamebaini ufanisi unadorora kwa kuwa zaidi ya wafanyakazi 120 wana elimu ya darasa la saba na zaidi ya 1,000 wameishia kidato cha nne. 
“Wale wote wenye tabia ya wizi, umangimeza, rushwa, ubadhilifu na ufisadi hawana nafasi,” alisema. 
Dk Ramadhani alisema shirika hilo linasuasua kutokana na wingi wa madeni na hadi Juni, 2016 lilikuwa linadaiwa Sh20.5 bilioni. Kati ya fedha hizo, Sh16 bilioni ni makato ya wafanyakazi yanayotakiwa kwenda Mamlaka ya Mapato (TRA). 
Pia, alisema TPC inaidai Serikali Sh5.5 bilioni, taasisi za umma Sh1.9 bilioni, watu binafsi Sh1.8 bilioni na hivyo kulitaka kuongeza juhudi katika kukusanya madeni.

0 comments:

Post a Comment