WABUNGE jana waliujia juu uongozi wa Bunge kwa kueleza kuwa hawako
tayari kukatwa Sh. 30,000 kila mmoja kwa ajili ya kumchangia mwakilishi
wa Tanzania katika mashindano ya ‘World Super Model’, Asha Ally Mabula.
Baadhi yao walisema michango bungeni imekuwa mingi sana, hivyo kama
watakatwa kiasi hicho cha fedha, watakwenda mahakamani kulishtaki Bunge
kwa kuwa kutoa mchango ni hiari na siyo lazima.
Walitoa msimamo huo baada ya Mbunge wa Urambo (CCM), Magreth Sitta,
kuomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Change, kuhusu
kumchangia mlimbwende huyo ambaye anakwenda kuiwakilisha Tanzania katika
visiwa vya Macau nchini China.
Sitta alisema ni vyema wabunge wakamchangia mrembo huyo kuanzia Sh.
30,000 kwa kuwa anakwenda kuiwakilisha Tanzania, jambo ambalo
litainufaisha nchi hususani katika sekta ya utalii.
Hoja hiyo ilizua mjadala mkali kwa wabunge na kusababisha mgawanyiko huku baadhi wakiunga mkono hoja hiyo na wengine wakiipinga.
Mmoja wa wabunge waliopinga vikali mchango huo ni Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema),Tundu Lissu, aliyesema hawezi kumchangia mlimbwende
huyo kwa kuwa hali ya chakula katika jimbo lake ni mbaya.
Lissu alisisitiza kutokuwa tayari kuchangia fedha hizo kwa kuwa licha ya
hali mbaya ya chakula jimboni kwake, pia kufanya hivyo ni hiari.
Mbunge wa Konde (CUF), Hatibu Said Haji, alisema hayuko tayari
kumchangia mrembo huyo kwa kuwa lengo la serikali ni kubana matumizi na
kutaka wizara husika ibebe jukumu hilo.
Alisema kwa mujibu wa dini yake ya kiislamu, hairuhusu kumchangia mtu kwa ajili ya kwenda kushiriki katika mashindano ya urembo.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Martha Mlata, alisema linapokuja suala la
kuchangiana kwa ajili ya harusi, wabunge wanalipa kipaumbele, lakini
linapokuja suala la kumchangia mtu kwa manufaa ya taifa wanakuwa wagumu
na kuongeza kuwa ni vizuri kumchangia Asha.
Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh, alisema hayuko tayari kukatwa kiasi chochote cha fedha kwa kuwa kutoa ni hiari.
Alisema kama kuna mbunge anahitaji kumchangia mlimbwende huyo, atoe mwenyewe kwa hiari yake.
Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi, alisema timu ya taifa ya
soka ya Vijana Serengeti Boys walipokwenda bungeni walichangiwa, hivyo
wabunge wanapaswa kutenda vivyo vivyo kwa mrembo huyo.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, alisema michango imezidi bungeni, hivyo siyo lazima kumchangia mtu.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keisy, alisema kumchangia mlimbwende huyo ni hiari, hivyo hayuko tayari kufanya hivyo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kumchangia mtu ni hiari na siyo lazima, mimi
siko tayari kukatwa hata senti tano, na endapo nikikatwa fedha zangu
nitakwenda mahakamani,” alisema Kessy.
Kutokana mgawanyiko huo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliwahoji
wabunge kwa kupiga kura ya wazi ya Ndiyo au Hapana. Hata hivyo, wabunge
waliomuunga mkono Sitta walishinda.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment