Friday, 28 April 2017

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imemwachia huru aliyekuwa mwenyekiti wa UVCCM Arusha Lengai Ole Sabaya baada ya Jamhuri kukosa ushahidi.

Na Wankyo Gati,,ARUSHA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, leo imemuachia huru aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Lengai Ole Sabaya baada ya kuona upande wa Jamuhuri wazembe wa kushindwa kuleta mashahidi katika kesi ya kujifanya Afisa Usalama wa Taifa (TISS).

Akisoma uamuzi wake jana uliotokana na ombi la Wakili wa Serikali Grace Madikenya la kuomba Mahakama hiyo kuiondoa kesi hiyo kwa sababu ya kukosa shahidi muhimu katika kesi hiyo na kupingwa na Upande wa Utetezi kuwa wanatumia vibaya mahakama kumtesa mteja wao, Gwantwa

Mwakuga, alisema Mahakama inasikitika kuona mwendesha mashitaka wa serikali, anatumia kigezo cha kuondoa kesi na kumkamata mshitakiwa kwa maslahi yake mwenyewe.

Alisema kesi hiyo imekuja mara ya pili baada ya kufunguliwa kesi namba 376/2016 na ilipofika katika utoaji wa ushahidi wa mpelelezi wa kesi hiyo, Mwendesha mashitaka aliomba Mahakama kuiondoa kesi hiyo kwa madai hawana nia ya kuendelea nayo na na mahakama ilikubaliana naye na kumwachia huru, lakini siku hiyo hiyo Desemba 14 Mshitakiwa alikamatwa.

“Kinachosikitisha Mahakama ilishuhudia kwa macho yake baada ya kumwachia mshitakiwa alipotoka nje alikamatwa tena na kuletwa tena Mahakamani hapa, kwa hakimu Mfawidhi Augustino Rwezile na mashitaka yalikuwa yale yale hakuna kilichorekebishwa na sasa wanaomba tena kuondoa kwa kigezo shahidi muhimu yupo nje ya nchi kwa miezi 18, hii ni utumiaji vibaya ofisi ya mwendesha mashitaka, ili kutesa watu,”alisema.

Gwantwa alisema Mahakama inatambua nguvu ya Mkurugenzi wa Mashitaka aliyonayo, lakini nguvu hiyo isitumike vibaya ni muhimu kuzingatia maslahi ya umma,haki na utedaji kazi wa Mahakama.Alisema Mahakama hiyo imejiuliza kipya kilichorekebishwa katika kesi hiyo ya pili namba 493/2016 na kuona hakuna, isipokuwa upande waJamuhuri wamefanya kwa kukidhi mataka yao wenyewe.

“Hapa upande wa jamuhuri wazembe wameshindwa kuleta mashahidi wakitakiwa kuleta wanaleta sababu wapo Kenya mara nje ya nchi, mara kuleta mashahidi ngumu, ili mradi kucheleesha kesi hii, mshitakiwa anazo haki zao za msingi za kuona kesi yake ikiendelea, lakini Jamuhuri inatesa Wadaawa kwa ajili ya maslahi yao, kitu ambacho mahakama hii haiko tayari kuona ikichezewa kwa namna hiyo,”alisema huku akinukuu kesi mbalimbali.

Alisema vema wadau wa Mahakama wakafahamu kuwa mahakama ni hekalu la kutenda haki kwa washitakiwa na walalamikaji sio vinginevyo na haki ya mshitakiwa kuona mashauri yafike mwisho na Mahakama haiwezi kuvumilia kuona mshitakiwa anakamatwa kwa kigezo cha kutumia mahakama vibaya.

Alimalizia kusema kimsingi kifungu cha 91 cha sheria ya mwendendo wa makosa ya Jinai ambacho upande wa Jamuhuri waliomba mahakama ikitumie kuondoa shauri hilo, inakikataa na kutumia kifungu cha 225 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kumwachia huru mshitakiwa huyo.

Awali kabla ya hakimu Gwantwa kuanza kusoma uamuzi huo, Wakili wa serikali, Grace Madikenya aliiambia mahakama hiyo haipo tayari kuendelea kusikiliza shauri hilo kwani tayari ameomba kuliondoa na lipo kinyume cha sheria, huku Wakili wa utetezi Charles Adiel akiomba Mahakama hiyo kusoma uamuzi wa mahakama kwa niaba ya mteja  wake na atapokea.

Sabaya mwaka jana alifikishwa Mahakamani hapo na kusomewa mashitaka mawili ambapo la kwanza ni kuwa Mei 18 mwaka 2016, katika Hotel ya Sky Motel, Mshitakiwa Sabaya alijifanya Afisa usalama wa Taifa (TISS) na kupata huduma ya kulala katika hotel hiyo, kwa kupata chakula navinywaji wakati sio kweli.

Shitaka la pili Sabaya anashitakiwa kughushi kitambulisho ya TISS kilichosomeka MT.86117 wakati akijuwa wazi kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Sabaya alikuwa akitetewa na Wakili Edna Haraka na Charles Adiel



Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment