KOREA KASKAZINI jana imesema itaonesha uwezo wake mkubwa wa kijeshi kwa
kuizamisha meli ya kubebea ndege za kivita ya Marekani iliyo njiani
kuelekea rasi ya Korea.
Kauli hiyo imekuja baada ya meli mbili za japani kuungana na ya Marekani kwa mazoezi ya kivita magharibi mwa Bahari ya Pasifiki.
Rais wa Marekani, Donald Trump aliamuru meli hiyo USS Carl Vinson
kuelekea katika rasi hiyo kufuatia majaribio ya makombora ya nyuklia ya
Korea Kaskazini na tishio la shambulio dhidi ya Marekani na washirika
wake wa Asia.
Marekani haijataja eneo hasa ambalo meli hiyo imefika, lakini Makamu wa
Rais wa Marekani, Mike Pence alisema itawasili ndani ya siku chache bila
kufafanua.
“Majeshi yetu ya mapinduzi yamejiandaa kuizamisha meli inayotumia nguvu
za nyuklia ya Marekani kwa pigo moja,” Rodong Sinmun, gazeti la chama
tawala cha Wafanyakazi nchini humo lilisema.
Gazeti hilo liliifananisha meli hiyo na ‘mnyama mchafu’ na kwamba pigo
hilo litaonesha mfano halisi wa uwezo wa kijeshi wa Korea Kaskazini.
Katika kinachoonekana ongezeko la mgogoro baina ya pande hizo mbili,
Korea Kaskazini imemkamata mtu mwenye asili ya Marekani na Korea na
kufanya idadi ya Wamarekani wanaoshikiliwa mjini Pyongyang kufikia
watatu.
Mtu huyo aliyejulikana kwa jina moja la Kim, amekuwa nchini humo kwa
mwezi moja kwa shughuli za hisani, shirika la habari la Yonhap limesema.
Alikamatwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa Pyongyang wakati akijiandaa kuondoka humo.
Taifa hilo linatarajia kuadhimisha miaka 85 ya kuwekwa msingi wa jeshi lake la watu wa Korea kesho.
Huko nyuma maadhimisho muhimu kama hayo yamekuwa yakiendana na majaribio ya silaha.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment