Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeibana Serikali kueleza kama Kivuko
cha MV Dar es Salaam kilichosanifiwa na kutengenezwa kwa ajili ya
kusafirisha abiria kinakidhi vigezo kwa matumizi ya kijeshi.
Kwa mujibu wa kambi hiyo, mwaka huu, Rais John Magufuli alitangaza kuwa
kivuko hicho amekigawa kwa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha
Wanamaji.
Kivuko hicho hujulikana kama ‘Kivuko cha Magufuli’ kwa sababu
kilinunuliwa wakati wa awamu ya nne alipokuwa Waziri wa Ujenzi kwa lengo
la kuondoa tatizo la usafiri kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo.
Mbunge wa Momba, (Chadema), David Silinde alitoa kauli hiyo bungeni jana
wakati akisoma maoni ya kambi ya upinzani kuhusu bajeti ya Wizara wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2017/18 kwa niaba ya
Waziri Kivuli wa wizara hiyo, James Mbatia.
Silinde alisema kwa mujibu wa Kumbukumbu Rasmi za Bunge, Serikali
ililiambia Bunge kuwa kivuko hicho hakikupokewa kwa sababu hakikuwa na
vigezo vya kimkataba.
Alisema Serikali ilisema badala yake, kampuni iliyoiuzia Tanzania kivuko
kile ilikuwa inakifanyia matengenezo ili kiweze kukidhi vigezo vya
kimkataba likiwamo tatizo la ‘speed’ ambalo lilikuwa kinyume na matakwa
ya kimkataba.
“Watanzania wanasubiri taarifa kama ukarabati wa kivuko kile umekamilika
na kama kivuko kile sasa rasmi kimekabidhiwa kwa Serikali,” alisema na
kuongeza:
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina tatizo na maamuzi hayo ya Rais
ikiwa lengo la kugawa kivuko hicho ni kurahisisha ulinzi na ‘patrol’
(doria) katika eneo la Bahari ya Hindi ili kudhibiti magendo na
uingizaji wa bidhaa haramu pamoja na wahamiaji haramu wanaotumia Pwani
na fukwe za Bahari ya Hindi kuingia ndani ya nchi,” alisema.
Alihoji ni lini marekebisho ya kivuko hicho yalikamilika na ni lini kivuko hicho kilikabidhiwa kwa Serikali.
Silinde alisema bajeti ya kununua kivuko hicho ililenga kuondoa tatizo
la usafiri kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo mkoani Pwani.
Kambi hiyo ilihoji Serikali imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya
kununua kivuko kingine ambacho kitafanya kazi ambayo ilikusudiwa
kufanywa na MV Dar es Salaam.
Kuhusu ukata
Silinde alisema kitendo cha Serikali kushindwa kutekeleza bajeti katika
kiwango kinachoridhisha ni matokeo ya vitendo vya Serikali kushindwa
kutekeleza miradi ambayo imepangwa kutekelezwa na Serikali yenyewe.
“Huu ni udhaifu mkubwa kama mpangaji wa mipango ni wewe na wewe ndiye
unashindwa kutoa fedha za utekelezaji, je, ni nani anatakiwa kutekeleza
mipango hiyo? Hoja ni masuala yasiyokuwa kwenye mipango kupewa nafasi
kubwa kuliko mipango iliyopangwa na kupitishwa na Bunge,” alisema.
Alisema kwa maneno mengine ni dharau kwa mhimili wa Bunge unaosimamia Serikali.
Silinde alisema fedha zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2017/18 ni
pungufu kwa Sh243.3 bilioni ukilinganisha na makadirio ya mpango wa
bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha
2016/17.
“Vipaumbele vya miradi vitakavyotekelezwa ni miradi inayoendelea
kutekelezwa, miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo na miradi
iliyopo kwenye Mpango wa Pili wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 hadi
2020/21.
Kambi hiyo iliishauri Serikali kuwa makini na kutekeleza vipaumbele kama
ambavyo vimepangwa na kwamba kutotekelezwa maana yake ni kuwa Bunge
lilitumia fedha na muda kama kivuli huku Serikali ikifahamu kuwa mpango
huo hautekelezeki.
“Kambi rasmi ya upinzani inaona ipo haja ya kudurusu mpango huo kama
unatekelezeka na pia haja ya kuwepo kwa sheria mahsusi ya kusimamia
mpango huo,” alisema.
Vibali vya ujenzi
Silinde alisema kitendo cha mkuu wa nchi kutoa kibali kwa baadhi ya
makandarasi bila kufuata taratibu za kutoa tenda (zabuni) kinaacha
maswali mengi ya kujiuliza hata kama Rais alikuwa na nia njema.
“Lakini sasa wananchi lazima wajiulize kuhusu Serikali yao kuna masilahi
gani na makandarasi waliopewa majukumu ya kukamilisha ujenzi wa miradi
hiyo? Je, umuhimu wa kuwa na sheria pamoja na taratibu za kusimamia
tenda za Serikali umesitishwa au hautumiki tena?” alihoji Silinde.
Alitoa mfano wa fedha zilizopatikana baada ya sherehe za Mwenge kuamriwa
kupelekwa kwenye ujenzi wa barabara ya Mwenge, ujenzi wa mabweni ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na ujenzi wa nyumba za Kota za
Magomeni.
Silinde alisema hadi kufikia Februari mwaka huu makandarasi na wahandisi
washauri walikuwa wanaidai Serikali takriban Sh788 bilioni
ikilinganishwa na deni lililokuwapo Juni 30 mwaka jana la takribani
Sh930 bilioni.
“Huu si utaratibu mzuri kwa Serikali kuendelea kuwakopa makandarasi
ilhali wameshamaliza na kukamilisha wajibu wao wa kimkataba na kwa wale
ambao hawajakamilisha miradi yao huongeza kasi ya utekelezaji kutokana
na namna Serikali imekuwa ikitoa fedha kwao,” alisema.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment