Siku moja baada ya TFF kuipoka Azam FC pointi tatu kutokana na kumtumia Erasto Nyoni aliyekuwa anakadi tatu za njano kwenye mchezo wao dhidi ya Mbeya City, kocha mkuu wa Azam FC Stewart Hall amefikia uamuzi wa kuachana na kikosi cha matajiri wa Dar baada ya kutokea kwa sekeseke hilo ambalo limeirudisha nyuma klabu ya Azam kwenye mbio za kuwania ubingwa wa ligi msimu huu.
“Baada ya jana kukatwa pointi na kupoteza matumaini ya ubingwa, Stewart Hall amethibitisha kwamba, ataachana na klabu ya Azam baada ya mchezo wa fainali ya kombe la FA dhidi ya Yanga”, zinasema ripoti kutoka ndani ya klabu ya Azam FC.
Stewart Hall ameuandikika barua uongozi wa Azam FC akiomba kujiuzulu nafasi yake mara baada ya kumalizika kwa msimu huu, sababu ambazo amezitaja Hall za kuamua kuachana na klabu hiyo ni kwamba, wachezaji hawamuelewi anachowaelekeza na haoni kama kuna maendeleo kadiri siku zinavyozidi kwenda.
Sababu nyingine iliyotajwa na kocha huyo raia wa England ni pamoja na aina ya wachezaji waliopo kwenye kikosi chake kutokidhi matakwa yake huku akidai haoni mustakabali wa baadaye ndani ya Azam FC.
Kwa mujibu wa habari kutoka TFF, katika mechi namba 156 iliyozikutanisha Mbeya City dhidi ya Azam kwenye uanja wa Sokoine, Mbeya, Azam FC ilimchezesha Erasto Nyoni akiwa na kadi tatu za njano kinyume na sheria huku wakitambua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
0 comments:
Post a Comment